Baba mzazi asimulia yaliyomkuta Masogange

Muktasari:

  • Masogange ni mtoto wanne katika familia yake ya watoto sita ambapo wakike ni watano.

BABA mzazi wa Agnes Masogange anayeitwa,  Gerald Waya amesema, mwanaye alikuwa nguzo katika maisha yao na kifo chake ni pigo kubwa kwake na familia kwa ujumla.

Waya amezungumza na MCL Digital nyumbani kwake Mbalizi  wilayani Mbeya, leo Jumapili na kusema,

Masogange ni mtoto wanne katika familia yake ya watoto sita ambapo wakike ni watano.

Amesema, Masogange amesoma Shule ya Msingi Utengule-Mbalizi na Sekondari ya Sangu akaishia kidato cha pili.

Waya amesema Masogange alipata matatizo hivyo akalazimika kuacha shule. Hata hivyo amesema hataki kuzungumzia mambo mabaya wakati huu anapoomboleza kifo cha mwanaye.

“Aliishia form two (kidato cha pili), akapata matatizo ikabidi aache shule. Tulikosana kidogo lakini tukayamaliza yeye akaenda Dar es Salaam,” amesema.

Waya amesema, “Mwanangu alikuwa nguvu kwangu, alikarabati nyumba hii ninayoishi kwa sasa na nilikuwa nafarijika sana, lakini leo kusikia msiba huu kwa kweli inaniuma sana.”

Amesema Masogange alimpigia simu, “Tukaongea naye akaniambia ‘mimi baba ninaumwa’.Nikamuuliza nini tatizo akasema, “aah!   baba niombee tu kwa Mungu’. Na Jumamosi iliyopita nilimpigia simu wakati yupo hospitali kujua maendeleo yake lakini akaniambia ‘baba byee’. Nikaanza kulia, na hapo sikuwasiliana naye tena hadi nilipopata taarifa za kifo chake,”amesema.