Utamu wa harusi ya Kiba uko hivi

Muktasari:

  • Kwa siku mbili za sherehe hiyo iliyoandaliwa katika Ukumbi wa Diamond Jubilee wa Mombasa, Mwanaspoti lilikita kambi na kufuatilia kila kitu kuanzia mwanzo hadi mwisho wa sherehe hiyo ya kukata na shoka.

ALHAMISI juma hili staa wa Bongo, Ali Saleh Kiba alikuwa nchini kufunga ndoa na mchumba wa Kikenya Amina Khalef Rikesh.

Ilikuwa ni sherehe ya kufana ambayo ni watu wachache sana wenye ukaribu na Kiba pamoja na familia ya mke ndio waliopata mwaliko.

Kwa siku mbili za sherehe hiyo iliyoandaliwa katika Ukumbi wa Diamond Jubilee wa Mombasa, Mwanaspoti lilikita kambi na kufuatilia kila kitu kuanzia mwanzo hadi mwisho wa sherehe hiyo ya kukata na shoka.

Kando na zile shamrashamra za harusi tu, Mwanaspoti lilibaini baadhi ya mambo ‘exclusive’ yaliyofungamana na matukio ya siku hiyo ya harusi.

HARUSI YAMKOSTI KIBA KSH50 MILLIONI

Ingawaje taarifa kutoka kwa upande wa Kiba zimearifu harusi ya pili kule kwao Dar es Salaam ndiyo itakayokuwa kubwa zaidi ya hiyo iliyofanyika hapa Kenya, ni dhahiri pia sherehe ya Mombasa yenyewe ilikuwa ya haiba yake.

Kulingana na mdokezi wetu ambaye ni mwanandani wa karibu sana wa Ali Kiba, sherehe nzima na harusi hiyo ya Mombasa ilikuwa yenye bajeti iliyofikia Ksh50 milioni.

“Ali pamoja na kusema harusi ya Kenya itakuwa ndogo, jamaa katumia mkwanja mrefu si haba. Nimefahamishwa hadi harusi inakamilika, Ali katumia karibia Ksh50 milioni kwa matumizi ya kulipia bili zote ikiwemo pia kulipa mahari,” mdokezi wetu alifichua kiasi hiki cha pesa kilijumuisha fedha alizolipa Kiba kwa wazazi wa kina msichana kama mahari, ununuzi wa vyakula, ukodishaji wa magari ya kifahari yaliyotumika kuwasafirisha wageni wake waalikwa kutoka sehemu moja hadi nyingine wakati wa sherehe hiyo,.

Malipo ya malazi ya Team ya Kiba Rockstar 4000 katika hoteli ya kifahari ya English Point Marina, ukodishaji wa Ukumbi wa Diamond Jubilee ambao unaarifiwa ulikosti Sh70,000 kukodisha kwa siku, gharama ya mapambo ya ukumbi huo unaosemekana ulifikia gharama ya Ksh2 milioni.

Vile vile kwenye hesabu za senti hizo, Kiba inasemekana alitumia kiasi kikubwa cha hela kuihamisha familia ya mke wake kutoka nyumba ya kawaida sana waliokuwa wakiishi pale Kongowea hadi kwenye nyumba yenye hadhi zaidi.

HONEYMOON NI ITALIA MWANA

Huku wengi mitandaoni na walioshuhudia jinsi shamrashamra za harusi hizo zilivyokwenda, kama ilivyo ada baada ya harusi lazima tu walioona waende fungate.

Kwa Kiba aka ‘Mr Privicacy’ kutokana na hulka yake ya kupenda kufanya mambo yake kimya kimya, mipango ya honeymoon ipo tayari japo ni taarifa ambazo amezibania mwenyewe na watu wake wa karibu.

Hata hivyo, upekuzi wetu umebaini Kiba tayari kapanga fungate yake na ni kumpeleka mpenzi wake Italia kwa muda wa kama wiki mbili hivi ili aweze kupunga upepo wa Ulaya kidogo na kuhisi kweli ameolewa.

Ni safari itakayomkosti kiasi zaidi cha pesa lakini Kiba anasemekana yupo radhi kufanya kila kitu kumpendezesha mkewe. Fungate itaanza mara tu baada ya harusi ya pili kule Dar.

KIBA NA MDOGO WAKE ABDU KUOA TENA SERENA

Taarifa zilizopo kule nje ni kwamba harusi za Kiba zitakuwa mbili, ile ambayo tayari ilishafanyika Mombasa na inayokuja ya Aprili 29 kule Dar es Salaam.

Hata hivyo, upekuzi wetu umebaini, bado kuna harusi mbili zaidi zitakazofuatia hiyo ya Mombasa.

Kesho Jumapili huko Dar, mdogo wake Kiba, Abdu Kiba naye atafunga ndoa na mchumba wake wa muda ambaye amekuwa akimweka siri. Ni siku ambayo pia Abdu ataachia ngoma yake mpya kwa ajili ya siku hiyo spesheli. Harusi hiyo kama ilivyo ada, Abdu atasindikizwa na kaka yake mkubwa Ali ikiwa ni kama vile kuurejesha mkono baada yake kumsindikiza kwenye harusi yake ya Mombasa.

Baada ya harusi yake Abdu hapo kesho, kaka hao watasubiri hadi Aprili 29 na watawaoa tena wake zao hao kwa pamoja katika hoteli ya kifahari ya Serena mjini Dar es Salaam.

Ndio sababu imetajwa itakuwa harusi kubwa zaidi ya iliyoshuhudiwa Kenya na taarifa tulizonazo ni gharama yake huenda ikawa mara mbili ya iliyotumika Mombasa.

KIKWETE, MASTAA KIBAO BONGO WAALIKWA

Tofauti sana na Kenya mastaa wachache wenzake Ali walioalikwa, harusi ya Dar inatazamiwa kupambwa na mastaa tupu wa Bongo Fleva.

Taarifa zetu zinatuarifu tayari kadi za mwaliko zimetumwa kwa Mbunge wa Mikumi Profesa Jay, AY, Mwana FA miongoni mwa wasanii wengine kibao pamoja na baadhi ya waandishi wa habari.

Mgeni wa heshima siku hiyo anatarajiwa kuwa Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ambaye Ali Kiba mwenyewe alimpelekea kadi ya mwaliko na familia yake mara tu aliporejea kutoka China alikokwenda kununua samani za kifahari za kumalizia mjengo wake wa nguvu ulioko Tabata, Dar es Salaam. Kama tu ilivyokuwa harusi ya Kenya, watoto hawataruhusiwa.

MKE WA KIBA KUACHA KAZI

MOMBASA

Zaidi ya picha zake mke wa Kiba kuzunguka mitandaoni kisha kubainika amekuwa akitoka na staa huyo kimyakimya kwa muda wa miaka miwili, mengi hayafahamiki kumhusu kichuna Amina Khalef Rikesh.

Upekuzi wetu umebaini, marehemu baba yake aliwahi kuwa diwani wa Mombasa. Aidha Amina mwenye umri wa miaka 23, amekuwa akifanya kazi katika Kaunti ya Mombasa ambayo gavana wake Ali Hassan Joho ni rafiki wa karibu sana wa Ali Kiba.

Kazi hiyo anaaminika aliunganishiwa na mdogo wake Joho, ambaye ana ukaribu sana na mama yake Amina.

kwa muda wote huo ambao amekuwa akitoka na Ali, Amina amekuwa akifanya kazi pale lakini sasa ataiacha na kuhamia Dar ili kuwa karibu zaidi na mume wake staa.

HARUSI YA KIBA YAMTOA JOHO UHISPANIA

Hadi kufikia Jumatano, baadhi ya vyombo vya habari vilikuwa vimeripoti gavana wa Mombasa ambaye ni rafiki mkubwa wa Kiba angeikosa harusi hiyo kwa sababu hakuwepo nchini.

Kwa muda wa miezi miwili, Joho amearifiwa kuwa Ulaya akifanya mambo yake na hadi inafikia harusi ya Kiba hakukuwa na taarifa za kurejea kwake. Hata hivyo, Joho hangeweza kuimisi harusi hiyo na anaripotiwa kutua Mombasa kimyakimya Jumatano usiku kutoka Ulaya.

“Joho hangeimisi harusi ya Ali, haingewezekana. Yaani mzee unaambiwa harusi hiyo ndio iliyomtoa Uhispania alikokuwa kwa zaidi ya miezi miwili. Aliingia kimya kimya kumpa sapoti msela wake,” mdokezi wetu aliongeza.

Gavana huyo na Ali wamekuwa na ukaribu sana tangu alipochaguliwa kwenye awamu ya kwanza na shoo nyingi alizopiga staa huyo wa Bongo huko Mombasa kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, zimekuwa zikidhaminiwa na Joho.

HARUSI YA KIBA ILIMLIPA

KSH9 MILIONI

Fedha hizo zilitokana na dili aliyosaini na Kituo cha Runinga cha Tanzania, Azam TV iliyonunua haki zote za kupeperusha matangazo hayo kwa fedha zinazoaminiwa kuwa takriban Tsh100 milioni (Ksh4.4 milioni) hadi Tsh200 milioni (Ksh9 milioni).

Hii ndio sababu ya Ali Kiba kujitahidi kuifanya harusi hiyo kuwa siri kubwa ili kuweza kulinda ule mkataba. Azam kwa upande wao, walipania kutengeneza hela kwa kuviuzia vituo vingine pamoja na kupitishia matangazo yao mengine kwenye matangazo yao.