Warembo hawa wamewavuruga mastaa wa soka!

Monday March 12 2018

 

KUTOKANA na kulipwa mishahara mikubwa, kuishi kwenye majumba ya kifahari na kuwa na maisha ya starehe, kimefanya kuwa chambo kwa wanasoka kukamatia mabinti warembo kabisa na kuanzisha nao uhusiano.

Kutokana na hilo mabinti hao wamekuwa hawajiweki mbali na wanasoka na kusababisha wengine kuamua kuwachanganya kabisa kwa kuwa na uhusiano zaidi ya staa mmoja wa soka, akiacha huyu anakwenda kumchukua yule.

Maisha hayo ya kulipwa mishahara kila wiki na si kulipwa tu, bali wanakunja mikwanja ya maana na hilo limekuwa kivutio kwa baadhi ya mademu kuamua kujisogeza kwa wanasoka hao ili kuwanasa na kuwaweka kwenye himaya yao ya kimapenzi. Lakini, kuna mademu wamepitiliza kwa kuwa na uhusiano wa wachezaji wa soka zaidi ya mmoja.

Elisabeth Reyes

Mrembo huyo, Elisabeth Reyes, ambaye ni mwanamitindo aliwahi kuwa Miss Hispania. Kitendo cha kuwa mrembo, kilimvuta beki wa Real Madrid, Sergio Ramos na kuanzisha naye uhusiano. Mrembo Elisabeth alikuwa kwenye uhusiano na Ramos kwa mwaka mmoja na baada ya hapo akaenda kuangukia kwenye penzi la mwanasoka mwingine, beki wa Getafe, Alexis Ruano. Hata hivyo, uhusiano huo haukudumu kwa muda mrefu sana. Elisabeth aliendelea kuwasaka wanasoka na hivyo kufanikiwa kumnasa staa wa Panathinaikos, Sergio Sanchez, ambaye huyu walimbeba jumla kwa kumuoa na walitarajia kupata mtoto mwaka jana.

Aida Yespica

Mrembo bomba, Aida Yespica. Aliwahi kushiriki shindano la ulimbwende la Miss Venezuela. Ndiyo, Miss Venezuela. Nadhani umeelewa. Mrembo Aida, alidaiwa kwamba ndiyo sababu iliyomfanya Real Madrid kuamua kumpiga bei Mesut Ozil kwenda Arsenal. Kwa mujibu wa ripoti ni kuwa Ozil alikuwa akicheza chini ya kiwango baada ya kunasa kwenye penzi la mrembo huyo, ambapo alikuwa hatulii Hispania, kwani muda wote alikuwa kiguu na njia kusafiri kwenda Italia kukutana na mrembo huyo. Lakini, mrembo huyo alikuwa na uhusiano na mwanasoka mwingine, beki wa Kitaliano, Matteo Ferrari, ambapo uhusiano wao wa miaka miwili ilileta matunda ya kupata mtoto wa kiume mwaka 2008.

Elisabetta Canalis

Elisabetta ni mwanamitindo wa Kitaliano, ambaye pia ni mwigizaji. Kabla ya hapo, mrembo huyo alikuwa mnenguaji. Baada ya kutambua fursa walionayo wanasoka ya kuvuna pesa za kutosha, mrembo Elisabetta hakusita kujiingiza kwenye uhusiano wa kimapenzi na straika wa zamani wa Inter Milan na Italia, Christian Vieri. Penzi hilo lilidumu kwa miaka minne hadi hapo walipokuja kuachana mwaka 2004. Mrembo Elisabetta akahamisha majeshi yake kwa mwanasoka mwingine, staa wa Kibrazili, Reginaldo Ferreira da Silva. Hiyo ilikuwa mwaka 2008 kabla ya kumwagana na kuwa gumzo kwenye vyombo vya habari alipoangulia kwenye penzi la mcheza sinema wa Hollywood, George Clooney. Hata hivyo, aliachana naye baada ya miaka miwili.

Nereida Gallardo

Mrembo Nereida Gallardo ni miongoni mwa mademu waliowachanganya wanasoka huko Ulaya. Mrembo huyo matata kabisa, aliwachanganya wachezaji wa timu moja, Sergio Ramos na mwenzake Cristiano Ronaldo huko Real Madrid. Nereida aliripotiwa kwanza kukutana na Ramos katika moja ya klabu za starehe za usiku huko Madrid. Hiyo ilikuwa mwaka 2007 na kipindi hicho Ramos alikuwa hajatulia kabisa. Mrembo Nereida alikuwa mtu wa kutoka sana usiku na ndipo alipokwenda kukutana na Ronaldo katika kumbi moja ya sterahe za usiku huko Mallorca. Hiyo ilikuwa mwaka 2008 na wawili hao walidumu kwa miezi michache na baada ya kuonekana wakiponda raha pamoja, ghafla kila kitu kikaenda kombo na kila mmoja akachukua njia zake.

Fanny Neguesha

Mrembo Fanny Neguesha, ambaye ni mwanamitindo alishafikia hata hatua ya kuchumbiana na straika Mario Balotelli na hiyo ilikuwa kabla ya fainali za Kombe la Dunia 2014 zilizofanyika huko Brazil. Wakati wengi wakidhani uhusiano huo utadumu kwa muda mrefu, ghafla kila kitu kilimalizika kilitibuna na Balotelli akampiga chini mrembo Fanny. Wakati kukiwa hakuna uhakika kama penzi hilo limevunjika, ikaibuka taarifa kwamba mrembo huyo anatoka na staa wa West Ham United, Cheikhou Kouyate baada ya kushea picha zao kwenye Instagram na walionekana wakifanya shopping huko Milan. Kufumba na kumfumbua, Fanny Neguesha ameangukia kwenye penzi la staa wa Gabon, mwanasoka huyo Mario Lemina, anayekipiga kwenye kikosi cha Southampton.

Melissa Satta

Mrembo, Melissa Satta, ambaye aliwahi kuwa maarufu kwenye vyombo habari baada ya kudai kwamba, kiungo Kevin-Prince Boateng anakuwa majeruhi mara kwa mara na haponi haraka kwa sababu anapenda sana ngono, kabla ya kuwa na uhusiano na staa huyo wa Ghana, Kevin-Prince Boateng alikuwa na straika wa Italia, Christian Vieri. Melissa na Vieri walikuwa kwenye mapenzi moto kati ya mwaka 2006 na 2011, lakini uhusiano wao ulivunjika. Mwaka 2011, Melissa akaangukia kwenye penzi la Kevin-Prince Boateng, aliyekuwa akiichezea AC Milan kipindi hicho. Wawili hao wamefanikiwa kupata mtoto mmoja wa kiume na wamedaiwa bado wapo kwenye penzi motomoto.

Raffaella Fico

Mwanamitindo wa nguvu, mrembo Raffaella Fico ameripotiwa kuwahi kuwa na uhusiano na supastaa wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo mwaka 2009. Lakini, muda mfupi tu baadaye, mrembo huyo akaanza kutoka na staa wa Italia, Mario Balotelli. Lakini, uhusiano wao ulikuja kuvunjika baada ya kuja kugundua kwamba fowadi huyo wa Nice, Balotelli anatoka na mwanamke mwingine, Jenny Thompson. Mrembo, Raffaella alitangaza kuwa mjamzito na kudai ni wa Balotelli, kabla ya straika huyo kukataa na kutaka wapime DNA jambo lililokuja kuthibitisha kwamba, Raffaella alikuwa akieleza ukweli.

Anara Atanes

Mrembo Anara Atanes alikuwa kwenye penzi la staa wa zamani wa Arsenal, Freddie Ljungberg kwa muda mrefu. Lakini, uhusiano wao ulikuja kuvunjika baada ya Anara kutuhumiwa kuchepuka na Keiran Richardson, aliyekuwa staa wa Manchester United. Richardson na Anara walionekana kwenye mtoko wa mlo wa usiku na kuzua maswali mengi hasa ukifahamika ukweli kwamba, huyo alikuwa akitoka na Ljungberg. Baadaye, Anara alihamia kwa mastaa wengine, akidaiwa kutoka na Darren Bent na Jermaine Pennant. Kwa sasa mrembo Anara yupo kwenye mahaba tele na staa wa Kifaransa, Samir Nasri tangu mwaka 2015.