Zile bao 4 za Simba, Dalali anahusika

Muktasari:

Dalali alisema zile shamrashamra za matawi zilikuwa zimeanza kupotea kutokana na mashabiki kuikatia tamaa timu hiyo, kwa kushindwa kuchukua ubingwa ndani ya miaka mitano, lakini alisema kwa sasa ameanza kurejesha moyo huo.

MWENYEKITI wa zamani wa Simba, Hassan Dalali, amejipa ujiko kwa kudai kuwa juhudi zake za kuhamasisha umoja na mshikamano katika matawi ya Simba nchini, zimeanza kuzaa matunda katika mechi yao ya Singida United waliyoshinda mabao 4-0 juzi Alhamisi.

Dalali alisema zile shamrashamra za matawi zilikuwa zimeanza kupotea kutokana na mashabiki kuikatia tamaa timu hiyo, kwa kushindwa kuchukua ubingwa ndani ya miaka mitano, lakini alisema kwa sasa ameanza kurejesha moyo huo.

“Pamoja na kwamba najitolea kwa ajili ya timu, bado kuna watu wanaochukia, sasa sijui hao wanaipenda Simba ipi, lengo langu ni kuona timu inakuwa na hamasa na tunaingia kwenye ushindani wa kucheza michuano ya kimataifa kupitia taji la Ligi Kuu Bara,” alisema.

“Hakuna ninachokihitaji klabuni zaidi ya kusonga mbele baada ya kuukosa ubingwa ndani ya miaka mitano mfululizo, hii sio desturi ya Simba, ndio maana tunahamasishana ili wanachama wawe na moyo wa kuiunga mkono timu yao na kuiombea mazuri badala ya mabaya.”

Dalali alisema ushindi wa juzi ni mwanzo tu, kwani amejipanga kuzunguka katika matawi yote ya Tanzania kwa gharama zake ili kuhakikisha matawi yaliyokufa yanaanza upya.

“Kwanza ifahamike naunga mkono juhudi za viongozi waliopo madarakani, sitaogopa changamoto kwa vile Simba nimeitumikia kwa uaminifu na mafanikio ya hali ya juu, hivyo lazima tukubali kujipanga na kujituma,” alisema.