Yondani awaonya Simba kuhusu ubingwa

Muktasari:

Simba ipo kileleni Ligi Kuu kwa pointi 26, ikifuatiwa na Azam (26) wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.

Mwanza. Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Mbuyi Yondani amesema licha ya Simba kuongoza Ligi Kuu kwa sasa, lakini kuna mambo kadhaa kama haitashtuka mapema basi isahau ubingwa.
Simba ipo kileleni Ligi Kuu kwa pointi 26, ikifuatiwa na Azam (26) wakitofautiana mabao ya kufunga na kufungwa.
 Yondani alisema  Simba ina matatizo kama haitabadilika mapema, basi ubingwa inaweza kuusikilizia bombani kwani imekosa mshauri anayejua soka katika benchi la ufundi.
 Alisema kuwa mbali na kumkosa mshauri, bado makocha wamekuwa wakifanya kazi kwa presha bila kuwa na uhuru sambamba na kukosa muunganiko imara kwa wachezaji.
 “Kwanza kitendo cha kumfukuza Omog (Joseph) katikati ya ligi ni moja ya tatizo, angalia sasa hivi hakuna kikosi cha kwanza cha kuaminika, kama hawatashtuka ubingwa watausoma namba”alisema Yondani.
 Nyota huyo wa Wekundu,aliongeza kuwa kwa mwenendo wa timu za Azam na Singida United unamvutia na kwamba iwapo zitaendelea hivi, basi mmoja wapo anaweza kutwaa ubingwa wa msimu huu.
 “Yanga nao sijaona kama wana kipya chochote, bado wanahitaji mabadiliko makubwa hawatofautiani sana na Simba, lakini Azam na Singida kidogo wanaonyesha kitu fulani kipya,”alisema mshambuliaji huyo.