Yes... ni Ajibu!

Pichani ni nyota wa Yanga  wakijifua kwenye mazoezi yao huko Shelisheli  Timu hiyo imefuzu raundi ya kwanza ya michuano yao ya barani Afrika. PICHA|CHARLES ABEL

Muktasari:

Yanga sasa itakutana na Township ya Botswana au El Merreikh ya Sudan zilizoumana usiku wa jana.

STRAIKA Ibrahim Ajibu jana Jumatano alifanya kile ambacho mashabiki wa Yanga walikuwa na hamu ya kukiona kutoka kwake, alipoivusha timu hiyo kuingia raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuing’oa St. Louis ya hapa Shelisheli.

Ajibu aliyeng’ara katika mchezo huo sambamba na Hassan Kessy, alifunga bao muhimu kwa Yanga sekunde chache kabla ya mapumziko na kama si wenyeji kubahatika kusawazisha katika muda wa nyongeza kufanya matokeo kuwa 1-1, Yanga ingekuwa imesonga kwa jumla ya mabao 2-0. Sasa imesonga kwa mabao 2-1.

Yanga sasa itakutana na Township ya Botswana au El Merreikh ya Sudan zilizoumana usiku wa jana.

Ikicheza bila nyota wake kadhaa walioachwa Tanzania kutokana na kuwa majeruhi, Yanga iliyokuwa ikipewa sapoti na kikundi cha Watanzania wanaoishi nchini hapa huku ikishuhudiwa na APR ya Rwanda ambayo nayo ilikuwa hapa kucheza mechi ya Kombe la Shirikisho,  ililianza pambano hilo kwa kasi na kusaka mabao ya mapema, lakini umakini wa kipa wa St. Louis uliifanya timu hiyo ikose mabao.

Ikitumia mfumo wa 3-5-2, Yanga iliwazidi maarifa wenyeji wao kwa mashambulizi makali ya pembeni kutoka kwa mabeki Kessy na Gadiel Michael, huku Ajibu, Emmanuel Martin na Pius Buswita wakiwakimbiza mabeki wa St. Louis.

Ndipo katika dakika ya 45 krosi murua ya Kessy ikaunganishwa wavuni na Ajibu na kuipa Yanga uongozi kabla ya kipindi cha pili wenyeji kuonekana kucharuka na kuliandama lango la Yanga lililolindwa vema na mabeki Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani na Kipa Youthe Rostand, lakini wakachomoa kwa bao hilo la jioni.

Katika kipindi hicho timu zote zilifanya mabadiliko, Yanga ikimtoa Gadiel, Said Juma ‘Makapu’ na kuwaingiza Haji Mwinyi na Rafael Daud huku wenyeji wakiwatoa Aglae na Melvin Mathiot na kuwaingiza Jude Nancy na Roddy Melanie.

Mabadiliko hayo yaliufanya mchezo kuwa fifte fifte kwa timu zote kufanya mashambulizi ya kupokezana, huku Yanga wakikosa mabao ya wazi kupitia kwa Ajibu na Rafael, huku mwamuzi Andofetra Rakotojaona kutoka Madagascar akiwa mkali kwa wachezaji waliokuwa wakipoteza muda uwanjani. Wakati mashabiki waliokuwa uwanjani wakiamini Yanga imetoka na ushindi wa bao 1-0, wenyeji kupitia Travis Lawrance ndio wakasawazisha kwenye dakika ya pili kati ya nne za nyongeza baada ya mabeki wa Yanga kujichanganya.

Lawrance aliunganisha kwa kichwa krosi ya Jude Nancy huku Yondani na Kessy wakishindwa kuondoa mpira huo uliompita kipa Rostand.

JKU YAPIGWA WIKI

Katika mechi nyingine ya michuano hiyo, wawakilishi wenginme wa Tanzania, JKU ya Zanzibar ilifumuliwa mabao 7-0 na Zesco ya Zambia huku Zimamoto ikitoka kwenye Kombe la Shirikisho kwa kulala 1-0 mbele ya Welayta Dicha ya Ethiopia na kutolewa kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya sare ya 1-1 nyumbani wiki iliyopita.

Wawakilishi hao wa visiwani wameaga rasmi michuano hiyo na kuziacha timu za Bara ikiwamo Simba iliyofuzu kwa kuing’oa Gendarmarie Nationale ya Djibout kwa jumla ya mabao 5-0 zikisonga mbele.

Yanga: Rostand, Kessy, Gadiel/Mwinyi, Yondani, Cannavaro, Makapu/Rafael, Pato. Tshishimbi, Ajibu, Buswita na Martin.