Yanga yamshtukia Chirwa

Muktasari:

  • Ndio, Chirwa kwa sasa amekuwa mtamu kinoma akitupia kambani kadiri anavyojisikia na kuifanya Yanga kuwa na matumaini ya kutetea ubingwa wa inaoushikilia mara tatu mfululizo.

MASHABIKI wa Yanga wanachekelea baada ya kuona pengo la pointi baina yao na vinara wa Ligi Kuu Bara Simba likipungua kutoka saba na kufikia tano, lakini mabosi wa klabu hiyo kuna kitu wamekishtukia kuhusiana na straika wao, Obrey Chirwa na kuchukua hatua fasta.

Ndio, Chirwa kwa sasa amekuwa mtamu kinoma akitupia kambani kadiri anavyojisikia na kuifanya Yanga kuwa na matumaini ya kutetea ubingwa wa inaoushikilia mara tatu mfululizo.

Mzambia huyo mpaka sasa ana mabao 11, matatu pungufu ya aliyonayo kinara wa mabao wa ligi hiyo, Emmanuel Okwi wa Simba mwenye 14.

Utamu wa Chirwa umewafanya hata wale waliokuwa wakimponda alipotupia picha akiwa shambani Zambia kutulia.

Ndio, watapiga kelele zipi wakati jamaa anaibeba timu yake, pengo la pointi limepungua na kuwapa ahueni mashabiki wa Jangwani kutembea kifua mbele wakiwapa kashkash watani zao Simba waliokuwa wakitamba sana Yanga ilipokuwa ikiyumba.

JANGWANI

WASHTUKA

Hata hivyo wakati mashabiki hao wakichekelea, mabosi wa Yanga wametuliza akili zao na kufuatilia mjadala kuhusiana na Chirwa kutakiwa na watani zao, Simba na kubaini mchezo mchafu na fasta wakaamua kufanya jambo ili kuukwepa mtego.

Mabosi wa Simba wamedaiwa kumnyapianyapia straika huyo ili atue Msimbazi na hasa kutokana na kuvutiwa na kasi yake ya kutupia kambani sambamba na usumbufu wake uwanjani, lakini Yanga inajua huo ni mtego kwao.

Straika huyo amesaliwa na mkataba mfupi kabla ya kuumaliza ule uliokuwapo na hivyo kuwa huru kuzungumza na klabu yoyote sasa kwa mujibu wa taratibu za usajili zilizotolewa na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Soka (Fifa), lile la Afrika (CAF) pamoja na la Tanzania (TFF).

Inaelezwa mkataba wa Chirwa umesaliwa na miezi minne, hivyo kitendo cha Simba kujitokeza kuanza kuonyesha nia ya kutaka kumbeba straika huyo, kwa mabosi wa Yanga wanajua ni mtego ambao kama hawatakuwa makini utawagharimu.

Kocha Msaidizi wa Simba, Masudi Djuma, alishawahi kunukuliwa na Mwanaspoti akisema kuwa na mchezaji kama Chirwa ni msaada mkubwa katika kikosi huku baadhi ya viongozi wa Msimbazi wakikiri wazi kuvutiwa na Mzambia huyo na kutaka kumchukua Mfungaji Bora huyo wa Kombe la FA msimu uliopita.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, mara nyingi amemjadili staa huyo na kuahidi kuwa msimu ujao lazima amvalishe jezi nyekundu, huku kwenye mitandao ya kijamii viongozi wengine wa Simba wakisisitiza Chirwa atawafaa kwa aina ya soka lake.

MNYIKA AFUNGUKA

Hata hivyo, Yanga imeshtukia janja katika majadiliano yanayoendelea kuhusu nyota huyo na kudai kuwa ni moja ya mbinu za watani zao Simba kutaka kuwatoa katika mstari wakati huu wakikimbiza mwizi kimya kimya kusaka taji la nne la ligi.

Akizungumza na Mwanaspoti Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, alisema wamekuwa wakishuhudia uwepo wa taarifa mbalimbali kwamba Simba imemsajili au kukaribia kumalizana na Chirwa, lakini wao wanauangalia uvumi huo kwa sura mbili kisha kuna kitu wamekishtukia.

Nyika alisema wanatambua ni kweli mkataba wa Chirwa unakaribia mwisho lakini jambo hilo haliwapi shida kwa kuwa tayari wamejipanga kumbakiza.

Bosi huyo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano inayohusika na kutengeneza mazingira mazuri ya timu kushinda mechi zake, amesema: “Tumekuwa tukisikia katika vyombo vya habari kwamba Chirwa anakaribia kutua Simba. Tunachojua ni kwamba Chirwa bado ana mkataba halali na timu yetu, atakayemsajili mwache amsajili.

“Tumeshazungumza na Chirwa na kuna mambo yake tunayafanyia kazi, kifupi ni mchezaji wetu, lakini tunachokiona katika uvumi huu ni akili ya wenzetu kututoa mchezoni tuanze kufikiria mambo ya mchezaji mmoja mmoja ili tujiondoe katika utulivu wa kutetea taji letu.”

Nyika aliongeza kusema Yanga inaongozwa na watu makini na kila jambo lao wanalifanya kwa akili za hali ya juu na ndio maana hawashtuki kwa mijadala kuhusu Chirwa kwani wanaamini mbinu zinazotumiwa na watani zao zimepitwa na wakati.

“Yanga kwa sasa akili yetu ni ubingwa, tunapambana kuhakikisha kikosi chetu kinashinda mechi zake. Kila mchezo ulio mbele yetu tuna mpango mkakati wake, tunaangalia mechi zetu tu hatuwezi kuangalia usajili kwa sasa kwani wakati mwafaka ukifika tutafanya hivyo,” alisisitiza Nyika.

Yanga ipo nafasi ya pili nyuma ya Simba ikiwa na alama 37, tano pungufu na ilizonazo Simba inayoongoza kwa pointi 42.