Yanga yalia hujuma mapema

Muktasari:

Yanga itacheza na St Louis katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika

Shelisheli. Yanga wamelazimika kusubiri kwa zaidi ya dakika 40 uwanjani baada ya kumaliza mazoezi yao jioni hii kutokana na kucheleweshewa basi wanalolitumia kwa safari zao tangu walipofika Shelisheli.

Mazoezi hayo ya saa mbili yalianza mnamo saa 9 alasiri na kumalizika saa 11 jioni kwa muda wa huku, lakini yalipomalizika walijikuta solemba baada ya basi hilo kutoonekana uwanjani hapo.

Kutokana na kuchelewa kwa basi hilo, viongozi wa Yanga, Samuel Lukumay na Hussein Nyika kwa kushirikiana na mwakilishi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Issah Bukuku walijitahidi kuwasiliana na uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Shelisheli (SFF) ili kuangalia uwezekano wa kutatua tatizo hilo.

Uongozi huo wa SFF waliitaka Yanga kuwa na subira huku wakiambiwa kwamba basi liko jirani na uwanjani hapo linakuja.

Hata hivyo Yanga walilazimika kusubiri kwa zaidi ya dakika 40 ndipo likaja basi lingine ambalo lilikuwa tofauti na lile la mwanzoni.

Maelezo waliyopewa ni kwamba basi la awali lilishindwa kufika uwanjani hapo kutokana na kupata hitilafu wakati lilipokuwa linakwenda kuwafuata.

"Hiki wanachokifanya sio sahihi na ni lazima tukilalamikie kwa sababu kiutaratibu basi linatakiwa kuwepo hapahapa likiwasubiri wachezaji baada ya kuwaleta," alisema mwakilishi wa TFF, Issah Bukuku wakati wa jitihada za kusaka usafiri wa kuirudisha timu hotelini.