Yanga yajibu mapigo ya Hans Poppe

Muktasari:

Beki huyo amekuwa mmoja ya wachezaji tegemeo katika safu ya ulinzi ya Yanga msimu huu

Dar es Salaam. JUZI kati klabu ya Simba kupitia Mwenyekiti wao wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe iliampa gari kama zawadi kiungo wake Said Ndemla kwa pasi zake mbili za mabao katika mchezo dhidi ya Singida, nao Yanga imeamua kujibu mapigo.

Yanga imeamua kumjibu Hans Poppe kupitia beki wao wa kati, Andrew Vincent 'Dante' kwa kuamua kumkabidhi naye ndinga fasta kutokana na kuridhika na kiwango chake cha soka tangu atue Jangwani.

Mabosi wa Yanga wamefuatilia kazi ya Dante na kugundua kwamba kwa sasa ni moja kati ya nguzo imara na kuamua kumpa zawadi ya kumfanya ajitume zaidi.

Vigogo hao wamemuita beki huyo na kumkabidhi 'ndinga' aina ya vista ambayo wakati wowote mtamuona nayo Dante mitaani akitamba nayo kutokana na kazi yake ilivyowakosha mabosi wa klabu hiyo.

Akizungumza na Mwanaspoti Dante alikiri tayari gari hiyo alishakabidhiwa tangu aliporudi kutoka Zanzibar huku akiwashukuru viongozi hao kwa kuona mchango wake.

Dante alisema ameambiwa kwamba hatua hiyo haishii kwake tu bali viongozi hao wanaendelea kufuatilia ufanisi wa kila mchezaji na zawadi kama hizo zitafuata kwa kila mchezaji atakyeonekana kuithamini klabu yao.

"Unajua walinipigia simu nikiwa Zanzibar katika michuano ya Kombe la Mapinduzi wakaniambia nikirudi niwatafute ili wanikabidhi ingawa wao walitaka wakati uleule nimtume mtu akalichukue hilo gari, lakini nikawaomba wasubiri nirudi," alisema.

"Walichoniambia kwamba wao wanafuatilia kiwango cha kila mchezaji na kwamba kila mchezaji atakayekuwa akifanya vizuri kwa kuibeba timu watakuwa wanatoa zawadi," alisema Dante aliyetua msimu uliopiota akitokea Mtibwa Sugar.