Yanga yasonga mbele Ligi ya Mabingwa Afrika

Muktasari:

Ibrahim Ajib aliipatia Yanga bao la kuongoza akiunganisha vyema krosi ya chinichini ya Hassan Kessy.

Shelisheli. Kikosi cha Yanga kimesonga mbele kwenye mashindano ya Klabu Bingwa Afrika baada ya kuifunga St. Luois ya Shelisheli jumla ya mabao 2-1.
Ibrahim Ajib aliipatia Yanga bao la kuongoza akiunganisha vyema krosi ya chinichini ya Hassan Kessy.
Awali krosi hiyo ilimpita Buswita lakini Ajibu akamalizia vyema na kuifanya timu hiyo ya Jangwani kumaliza mchezo huo kwa sare ya 1-1 dhidi ya St. Louis.
Mchezo wa awali uliopigwa jijini Dar es Salaam, vijana wa Kocha George Lwandamina walifanikiwa kuifunga St. Louis bao 1-0.
Upande wa St. Louis walicheza mchezo wa nguvu kipindi cha kwanza hata hivyo safu ya ulinzi Yanga ilikuwa thabiti kuzuia hatari zote.
Yanga imeifuata Simba ambayo imetangulia jana baada ya kushinda mchezo wake wa kimataifa wa Kombe la Shirikisho ikiiondoa Gendermarie kwa jumla ya mabao 5-0.