Yanga yaifuata Rollers kibabe

Muktasari:

Mabingwa hao bado wanasumbuliwa na majeruhi katika kikosi chake cha kwanza


Dar es Salaam.Baada ya kuichapa 3-1 Stand United, Yanga wanaondoka leo usiku wa saa nane kuelekea Botswana tayari kwa mchezo wa marudiano dhidi ya Township Rollers.

Yanga wanaenda Botswana wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa 2-1 katika mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam, hivyo wanahitaji ushindi wa bao 1-0 ili kusonga mbele kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Katika mchezo dhidi ya Stand, Yanga ilifunga mabao yake mapema ambayo yaliwanyong'onyesha kabisa wapinzani wao ambao walipoteana katika kipindi cha kwanza.

Mabao ya Yanga yalifungwa na Ibrahim Ajib, bao la kujifunga kwa beki wa Stand United, Ali Ali na Obrey Chirwa huku Vitalis Mayanga akifunga bao la kufutia machozi kwa Stand.

 

Katika kipindi cha pili Stand walionekana kubadilika na kupata bao kupitia kwa Vitalis Mayanga lakini Yanga walimaliza shughuli baada ya Obrey Chirwa kufunga bao la tatu.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 46, sawa na Simba inayoongoza kwa tofauti ya mabao wakati timu hizo mbili zikigeukia katika mashindano ya kimataifa mwishoni wiki.

Kocha wa Stand, Athuman Bilal 'Bilo", alisema wachezaji wake walishindwa kutumia vizuri kipindi cha kwanza na ndiyo sababu ya kupata matokeo mabaya.

"Wachezaji walipoteana na tulicheza dakika kumi na tano tu katika kipindi cha kwanza, mapumziko tuliongea nao ndio maana uliwaona wamebadilika na kupata bao," alisema Bilo.