Yanga yaibuka na zali, yaipiga bao Simba

SIMBA na Yanga zimesonga mbele katika mashindano ya klabu barani Afrika, lakini habari kubwa ni kwamba Wana Jangwani wamepata zali la maana.

Yanga ambayo itakutana na Township Rollers ya Botswana katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, imepata bahati kwani hata ikiondoshwa kwenye hatua hiyo itaangukia Kombe la Shirikisho iliko Simba kucheza mechi maalumu za kufuzu hatua ya makundi.

Mabingwa hao wa kihistoria wa Ligi Kuu Bara, wakifanikiwa kuwatoa Rollers watatinga makundi ya Ligi ya Mabingwa, ambapo watajihakikishia kiasi cha Sh1.1 bilioni kutoka Shirikisho la Soka la Afrika (CAF).

Hali ni ngumu kwa Simba kwani ikitolewa na Al Masry ya Misri haitakutana na mteremko ambao, Yanga imekutana nao.

Endapo Simba itafanikiwa kupiga hesabu zake vyema na kuwang’oa Waarabu hao, itabakiza hatua moja ili kufuzu ya makundi, lakini ikitolewa habari itaishia hapo na kugeukia VPL.

YANGA YAPANIA

Katika hatua nyingine, Yanga baada ya kubaini kwamba wapinzani wao sasa ni Township Rollers, wametabasamu na mabosi wa Jangwani wamewaambia mashabiki wao wakae mkao wa kula kwani, kazi imeanza.

Kwa mujibu wa ratiba ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga itaanzia nyumbani Machi 7 kabla ya timu hizo kurudiana Machi 16 huko Gaborone, Botswana.

Mshindi wa mchezo huo atafanikiwa kufuzu hatua ya makundi ya mashindano hayo, huku akijipatia kitita hicho (Sh1.1 Bilioni).

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Hussein Nyika, amesema wapo tayari kukabiliana na timu yoyote, hivyo hawana wasiwasi wowote na Wabotswana hao.

“Haya ni mapambano, unavyovuka hatua moja unajipanga kwa hatua nyingine. Hatua tunayokwenda ni ngumu zaidi, lakini niwahakikishie Wana Yanga kwamba tutajipanga na kujiandaa kikamilifu ili tuweze kuvuka na kuingia hatua ya makundi ambayo ndio lengo letu kuu,” alisema Nyika.

Beki wa timu hiyo, Hassan Kessy, alisema wana uzoefu wa kucheza mechi za Ligi ya Mabingwa, hivyo hawana hofu ya kukabiliana na timu yoyote ile.

“Sisi tuko tayari kucheza na ambaye atakuja mbele yetu kwa sababu tumewahi kukutana na timu nyingi ngumu na tulifanikiwa kuzitoa,” alisema.

“Naamini kila mmoja wetu anatambua jukumu lililo mbele yetu na tutaanza maandalizi mapema ya kuhakikisha tunapata matokeo mazuri yatakayotuvusha kwenda hatua inayofuata.”

Mara ya mwisho Yanga kufika hatua ya makundi kwenye mashindano ya kimataifa ilikuwa ni mwaka 2016 kwenye Kombe la Shirikisho Afrika.