Yanga yadondosha mojamoja

Dar es Salaam. LICHA ya kupata ushindi kiduchu mbele ya Ruvu Shooting, lakini mashabiki wa Yanga angalau jana wametoka Uwanja wa Taifa wakiwa na tabasamu, huku Azam FC ikikwea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara japo kwa muda.

Azam ilipata ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya timu ngumu ya Prisons, wakati Yanga ikiwa jijini Dar es Salaam ikiitambia tena Ruvu kwa kuilaza bao 1-0 na kuendeleza rekodi yao ya kujipigia tu maafande hao kutoka Mlandizi, Pwani.

Yanga imepata ushindi wa kwanza tangu waliponyooshwa na Mbao FC jijini Mwanza kisa kung'ang'aniwa na Mwadui wiki iliyopita kwa kulazimishwa suluhu, huku pongezi zikienda kwa Pius Buswita aliyefunga kwa kichwa dakika ya 43, akimalizia pasi krosi murua ya Ajib.

Hilo lilikuwa pambano la 13 kwa timu hizo kukutana katika Ligi Kuu Bara tangu mwaka 2010 ambapo Yanga imeshinda mara 12 na kulazimishwa sare mara moja tu.

Katika pambano la jana Yanga ilishindwa kuonyesha makeke yake, licha ya Ibrahim Ajib, Kabamba Tshishimbi, Amissi Tambwe na nyota wake wengine kushuka uwanjani, huku Ruvu ikikosa mabao mengi ya wazi ambayo yangewaondolea aibu.

Kwa ushindi huo Yanga imerejea nafasi ya tatu ikifikisha alama 25 kama ilizonazo Mtibwa Sugar ila faida ya mabao ya kufunga na kufungwa, ikiwa nyuma ya Simba ambayo imeshushwa na Azam iliyopata ushindi wa mabao 2-0 ugenini dhidi ya Prisons. Mabao ya Azam yalifungwa na Yahya Zayd dakika ya 70 na Paul Peter aliyefunga dakika ya 82, huku Mwadui ililazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Ndanda.