Yanga kicheko, gari limewaka

Muktasari:

Yanga ilikuwa haijapata ushindi wowote katika Ligi Kuu Bara kwa siku 61 tangu ilipoinyoosha Mbeya City kwa mabao 5-0 katika mechi ya Novemba 19 mwaka jana kabla ya juzi Jumapili kuifunga Ruvu bao 1-0.

MASHABIKI wa Yanga walikuwa hawana raha kutokana na chama lao kusuasua katika mechi zao za Ligi Kuu Bara, lakini ushindi wa juzi dhidi ya Ruvu Shooting umewapa mzuka huku benchi la ufundi likiwataka watulie kwani gari lao limewaka.

Yanga ilikuwa haijapata ushindi wowote katika Ligi Kuu Bara kwa siku 61 tangu ilipoinyoosha Mbeya City kwa mabao 5-0 katika mechi ya Novemba 19 mwaka jana kabla ya juzi Jumapili kuifunga Ruvu bao 1-0.

Ushindi huo umewapa faraja Wana Yanga huku benchi la ufundi pamoja na nahodha wa timu hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wakiwaahidi mashabiki wao juu ya kuendelea kuwapa raha hasa wakielekea kuvaana na Azam Jumamosi.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, aliliambia Mwanaspoti kuwa, timu yao imekuwa ikisuasua kutokana na ufiti mdogo wa wachezaji na kuwepo kwa tatizo la majeruhi wengi wa kikosi cha kwanza, lakini sasa kila kitu kipo vema.

Alisema benchi lao linaendelea kuwapika vijana wake ili kuweza kuendeleza raha Jangwani kwa kupata ushindi katika mechi hiyo ya kufungia duru la kwanza itakayochezwa Uwanja wa Azam Complex, wikiendi hii.

Yanga imekuwa ikiwakosa washambuliaji wake tegemeo akiwamo Donald Ngoma na Geofrey Mwashiuya walio majeruhi na Obrey Chirwa aliyesimamishwa kucheza kwa utovu wa nidhamu, pia ikikosa huduma za Thabani Kamusoko aliye majeruhi.

Kamusoko tayari ameanza mazoezi mepesi, lakini Nsajigwa anaendelea kuandaa vijana kwa michezo ijayo ili kuendelea kuwapa raha mashabiki wao, huku akitetea aina ya uchezaji wa vijana wake katika mechi ya juzi.

“Sisi kama benchi la ufundi tunaridhika kwa asilimia mia moja na kiwango cha ufiti kwa wachezaji wetu, hivyo hatuna wasiwasi hata kidogo. Kilichotokea dhidi ya Ruvu ni jambo la kawaida kwenye soka. Katika mechi dhidi ya Azam tutaingia kwa staili nyingine tofauti kabisa na ya mechi iliyopita,” alisema Nsajigwa ambaye timu yake ilipoteza nafasi kadhaa za mabao.

Cannavaro afunguka

Nahodha wa Jangwani hapo, Cannavaro, licha ya kushukuru ushindi wa juzi, pia alifichua kuwa kazi imeanza Jangwani, lakini akitaka mambo yanayoizingua timu hiyo yarekebishwe mapema ili kila kitu kiwe sawa mbele ya safari.

Cannavaro alisema hali ya kujiamini kwa wachezaji imejerea upya baada ya Yanga kukaa muda mrefu bila kushinda na mechi zao zijazo watazidi kuwanyoosha wapinzani wao.

“Tumesahau yote ya nyuma na sasa tunaangalia mechi zilizopo mbele yetu, morali imerejea kikosini na waliokuwa wanatuchukulia poa wajiandae kuumia sasa,” aliema.

Cannavaro alifichua pia kuwa uchanga wa wachezaji wengi wa kikosi chao ulichangia pia timu yao kutofanya vizuri na kutoa rai mabosi wao wajipange kufanya usajili wachezaji wazoefu kuondokana na tatizo la sasa.

“Sawa uongozi haukufanya vibaya kusajili vijana, ni wachezaji wazuri, lakini wanahitaji muda, kinachotumaliza sasa ni timu kuhitaji matokeo mazuri sasa, ndio maana presha inakuwa kubwa kwa vijana kushindwa kuibeba,” alisema.