Yanga, Stand ziwe makini, la sivyo zitazama

Muktasari:

  • Bila kujali kama taarifa hiyo imetengenezwa kwa sababu maalumu ama ni kweli Manji anataka kuachia ama anatingisha tu kiberiti. Mwanaspoti linataka kutoa rai kwa wanachama na viongozi wa Yanga kuwa makini.

WANACHAMA wa Yanga wametaharuki. Hii ni baada ya kusikia tetesi kwamba mwenyekiti wao, Yusuf Manji anataka kujiuluzu klabuni. Japo mpaka sasa Manji hajajitokeza kuweka bayana juu ya maamuzi hayo zaidi ya kusemewa na wengine, lakini wanachama na hata baadhi ya viongozi wameonyesha kupagawa.

Bila kujali kama taarifa hiyo imetengenezwa kwa sababu maalumu ama ni kweli Manji anataka kuachia ama anatingisha tu kiberiti. Mwanaspoti linataka kutoa rai kwa wanachama na viongozi wa Yanga kuwa makini.

Mihemko walionayo sasa na kuanza kunyoosheana vidole na kusimamishana haiwezi kuijenga timu yao. Hata kama kuna usaliti miongoni mwao, bado wanapaswa kuliendea jambo hilo kwa umakini na busara kubwa badala ya kuanza kutibuana wenyewe kwa wenyewe kwani siku zote, vita ya panzi ni tijara kwa mvuvi.

Kipindi kama hiki cha kuelekea kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu Bara ambayo itaanza Jumamosi ni lazima klabu yoyote sio Yanga tu, iwe na utulivu, amani na mshikamano wa dhati.

Hali ya vurugu, msuguano ama mgogoro wowote ni mwanzo wa timu kufanya vibaya na kutoa mwanya kwa wapinzani wao kuweza kupeta. Tuliona ndani ya Simba kwa misimu ya hivi karibuni wakati uongozi mpya wa Rais Evans Aveva ukiingia madarakani baada ya kuwasimamisha baadhi ya wanachama wao.

Simba ilikuwa ikifanya vibaya katika mechi zao za misimu miwili iliyopita kwa kile ambacho hata kama hakikuwa na ukweli ndani yake, lakini kilihusishwa na Kundi la Simba Ukawa ambalo lilitofautiana na uongozi wa Aveva.

Hata miaka kadhaa nyuma ndani ya Simba na Yanga yenyewe hali ya vurugu na kukosekana kwa mshikamano kulizifanya ziyumbe na kuchemsha katika ligi na michuano ya kimataifa, kuonyesha ubaya wa migogoro klabuni.

Hivyo kabla mambo hayajazidi kutibuka Yanga, lazima wanachama na viongozi wao wakaliangalia hilo na kuchukua hatua za haraka kuweka mambo sawa, ili baadaye kusiwe na wa kulaumiwa kwani kila mchuma janga hula na wakwao!

Rai kama hiyo pia Mwanaspoti inaelekeza kwa Klabu ya Stand United ambayo tangu mwishoni mwa msimu uliopita imekuwa kwenye mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe kiasi cha kumtisha hata mdhamini wao, Kampuni ya Acacia.

Wadhamini hao wametoa notisi ya miezi mitatu ili Stand ijipange na kumaliza tatizo lao kabla hajachukua maamuzi ya kujiondoa. Hilo litakuwa pigo kwa klabu hiyo na wadau wa soka wa Mkoa wa Shinyanga.

Uwepo wa Stand katika Ligi Kuu ni jambo muhimu kuliko migogoro inayoendelea klabuni hapo. Ndio maana tunasihi pande zinazosigana kukaa chini na kuangalia mustakabali wa timu yao.

Kama hawatamaliza tatizo lao basi wasitarajie miujiza zaidi ya kurudi mchangani.

Tunaamini wanachama na mabosi wa Yanga na Stand ni watu wenye upeo mkubwa na kutambua ubaya wa vurugu na mitafaruku baina yao, hivyo kukaa chini na kuangalia kipi bora, kumaliza migogoro mapema ama wasubiri waje wajute mbeleni mambo yakishaenda harijojo?

Siku zote kinga ni bora kuliko tiba, klabu hizo zinaweza kuamua sasa zisuke ama kunyoa, lakini zikiangalia faida na hasara ya kukumbatia migogoro inayoendelea kufukuta katika klabu zao ambayo imeanza kipindi kibaya.