Yanga, Simba wampa mzuka Kipa wa Stand Utd

Mwanza. Kipa wa Stand United, Mohamed Makaka amesema ndoto yake haitokamilika mpaka aone siku moja amejiunga katika klabu ya Simba au Yanga ambazo amesema angalau hapo atakuwa amepiga hatua kwenye soka.

Makaka amekuwa msaada mkubwa ndani ya kikosi cha Stand United msimu huu ambapo ubora wake langoni kumefanya kipa Frank Muwonge kupokonywa namba.

Akizungumza na gazeti hili,Makaka alisema bado malengo yake kwenye  mpira wa miguu hayajafanikiwa kwani anatamani siku moja kuona anacheza katika klabu kubwa za soka hapa Bongo.

“Kila mchezaji ana malengo yake kwenye soka mimi ndoto yangu ni kuona siku moja nachezea katika klabu za Simba au Yanga”alisema Makaka.

Kipa huyo alisema kwa sasa ana mkataba na Stand United ambapo lengo lake ni kuhakikisha anaibakisha Ligi Kuu timu hiyo msimu ujao.

“Sasa tunapambana kuona timu inabaki Ligi Kuu tena tukiwa katika nafasi tano za juu kwenye msimamo japo ushindani umekuwa mkubwa hilo halitupi presha sana”alisema Kipa huyo.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo,Agustino Malindi alisema kila kukicha kiwango cha kipa huyo kinaimarika jambo ambalo amesema kama akiendelea hivyo atakuwa moja ya walinda mlango bora hapa bongo.

“Anajituma sana kuanzia kwenye mechi hadi mazoezini ndio maana unaona anafanya vizuri kwa sasa kwenye Ligi na akiendelea hivi basi iko siku atakuja kuwa kipa bora kikubwa ajitume zaidi”alisema Malindi.