Yakub anaishi kisela kinoma

Tuesday February 13 2018

 

By Thomas Ng’itu

Dar es Salaam.Mpaka Home kama kawaida yake ya kutembelea watu, Jumatatu ya ipo na beki kisiki wa Azam FC, Yakub Mohammed, anayeishi Mbagala Chamazi, jijini Dar es Salaam. Mpaka Home alipofika kwa beki huyo, alimkuta akiwa ametulia ndani ya mjengo wake bila ya wasiwasi.

Mpaka Home ilitaka kufahamu mambo mbalimbali kuhusu Mghana huyo, tangu ajiunge na Wana Lambalamba hao waliojichimbia hapo Chamazi kukimbia vurugu za katikati ya jiji.

ANAISHI KISELA

Wanasoka wengi wa kigeni wakija Tanzania huwa wanapenda kuishi kifahari kwa maana na kukaa katika nyumba za kisasa na kutembelea magari ya kifahari, lakini kwa beki huyu hali ni tofatuti. Hapo kwake maisha ameyaweka kawaida sana.

“Ninaishi hapa mwenyewe kwa hiyo sioni kama kuna sababu kubwa ya mimi kuwa na vitu vingi ndani, ndio maana unaona sina mambo mengi, pia muda mwingi nautumia kukaa kambini, nikitaka kwenda mazoezini nampigia boda boda wangu anakuja kunichukua,” anasema.

Yakub anaongeza kwamba, akirudi kutoka kambini huwa anajifungia mapema ndani kwa sababu licha ya kwamba nyumba yake inapakana na Salmin Hoza, lakini kila mchezaji anakuwa kivyake kwani wakirudi wanakuwa wamechoka hivyo huhitaji kupumzika.

YEYE WALI NYAMA TU

Kitu ambacho huwa kigumu kuzoeleka kwa wengi unapokuwa ugenini, ni chakula kwani wengi hushindwa kula vyakula vya kigeni. Kwa Yakub hakuna tofauti sana.

“Chakula ni changamoto kwangu, hapa napika wali kwa kutumia mchele wa Kihindi, huu ni tofauti kabisa na mchele wa hapa kwenu, pale tunapoenda kucheza mikoani huwa napata tabu sana kiasi cha kulazimika kula mishikaki tu ili niwe sawa,” anasimulia.

Kuhusu nani huwa anampikia hapo nyumbani, anasema: “Napenda sana kupika mwenyewe, hata kule nyumbani Ghana huwa najipikia. Ninaamini kuwa chakula ninachopika mwenyewe ni kitamu kuliko cha kupikiwa. Nikiwa kamini ndio huwa  natumia chakula cha klabu, wao nao wanapika vizuri.”

RATIBA YAKE SASA

Unajua kuna watu hawana kabisa ratiba za mambo yao, yaani wao inavyokuwa ndio hivyo hivyo.

Yakub yeye ni mchezaji wa kulipwa, anaishi kwa ratiba hata anapokuwa nyumbani.

“Tukitoka mazoezini au kwenye mechi za hapa Dar, huwa narudi nyumbani kulala, mara chache hulala klabuni. Katika muda mwingine wa kupumzika hupenda kuangalia sinema, si mzururaji ila mara moja moja hutoka kama vile kwenda kwa James Kotei kupiga stori,” anasema.

SIMBA, YANGA, SINGIDA ZIMSAHAU

Wachezaji wengi hupenda kuzichezea Simba, Yanga na hivi sasa Singida United kwa vile zina pesa na kupata jina kubwa, lakini kwa Yakub ni tofauti.

“Siwezi kuondoka Azam kwa sababu ya timu hizo. Hapa ninapata kila kitu, hata mashabiki wake ni wa kweli na tukipoteza utaona kabisa wanaumia, siwezi kutoka hapa na nikaenda klabu hizo,” anasema.

“Ninacheza Azam kwa kujituma ili nikitoka hapa niende nchi nyingine iliyo juu kisoka zaidi ya Tanzania na Ghana. Najituma ili ukifika muda wa kuondoka basi  biashara iwe nzuri, kwangu na kwa Azam pia.”

RASTA ZAKE SIMPO TU

Ukiiangalia safu ya ulinzi ya Azam, lazima utakiona kidume kimoja kimesimama kikiwa na rasta nyingi hivi pamoja na ndevu za kutosha, ndiye yeye.

Anasema alianza kuzifuga rasta mwaka 2013 akiwa katika timu ya vijana ya Ghana walipokwenda Morocco.

“Kule kila mchezaji aliamua kuwa na staili yake ya nywele, mimi ndio nikachagua rasta,” anasema.

“Ninazihudumia kikawaida sana, natumia Shampoo pamoja na black ambayo naiweka nikiwa kambini au nyumbani. Sina mambo mengi, kikubwa nahakikisha tu ziwe safi. Ila nikienda mechi za ugenini ambazo ni za mfululizo huwa napata tabu ya muda wa kuziosha, kama umenifuatilia hubadilika mpaka rangi.”

KUMBE MUUZA CHENJI PIA

Umeshtuka? Ndio ipo hivyo. Yakub akiwa kwao mara nyingi hufanya biashara ya kubadili fedha akisema hata familia yake imewekeza upande huo.

“Nyumbani wote tunajihusisha na biashara hii, kuna kaka yangu ndio husimamia, nikipata pesa zangu huwa nazituma zinaenda kuzungushia humo, ni biashara nzuri na inalipa kiukweli,” anasema.

Lakini anasema soka limemfanya amiliki nyumba mbili kwao akiwa pia na mipango mingi ya baadaye.

AWAPOTEZEA MADEMU WA BONGO

Jamaa kutokana na kujifungia kwake, amekuwa akipishana na wale mademu wanaowawinda wachezaji maarufu ili kula nao bata.

“Ninawakwepa kabisa kwa vile nina mchumba wangu ambaye bado ni mdogo, yupo chuo anasomea mambo ya urembo. Ninampenda sana kwa sababu mimi ndio namlipia ada, siwezi kuchepuka kwa mtu mwingine wakati tayari nina mtu ambaye namjali, nataka akimaliza tu chuo nifunge naye ndoa tuanzishe familia,” anasema.