Wenger bado yupo sana Arsenal

Muktasari:

Mfaransa huyo ameifundisha Arsenal kwa zaidi ya miaka 20 sasa

London, England. Arsene Wenger amesema ataendelea kuwa Arsenal hadi mwisho wa mkataba wake.

Mfaransa huyo amesaini mkataba wa miaka miwili  msimu uliopita wa kuendelea kuifundisha Gunners pamoja na kuwepo kwa maandamo ya mashabiki wakimtaka ajiuzuru.

Wenger mara ya mwisho kuwapa ubingwa Arsenal ubingwa wa Ligi Kuu ilikuwa 2004 na mashabiki wengi wanataka kocha mpya wa kuifundisha timu hiyo.

Hata hivyo, mataji matatu ya Kombe la FA katika miaka minne yalitosha kumfanya kocha huyo mwenye miaka 68, kuendelea kubaki katika nafasi hiyo.

Akizungumza na beIN Sports, Wenger alisema: “Wakati wote nimekuwa nikiheshimu mkataba wangu.

“Ningependa kukumbusha kuwa nilisema hapana mara kadhaa kwa klabu kubwa duniani kwa sababu ya kuheshimu mkataba wangu wakati wote.

“Baada ya hapo tunatakiwa kufanya kazi mambo ya mbeleni na kuangalia namna ya timu kufanya vizuri.

“Tunatakiwa kucheza vizuri kila mchezo wa mbele yetu na kuhakikisha mwisho wa msimu tunafanya vizuri na kushinda mataji.

Tangu aliposaini mkataba mpya mwaka jana, Wenger amekuwa akitumia fedha kununua wachezaji wenye majina kwa lengo la kujenga kikosi chake.

Amevunja rekodi ya uhamisho wa klabu hiyo kwa kumsajili Alexandre Lacazette msimu uliopita kabla ya kutumia tena fedha mwezi uliopita kwa kuwasajili Pierre-Emerick Aubameyang pamoja na Henrikh Mkhitaryan.