Wenger aifuata Spurs kibabe

Friday February 9 2018

 

LONDON, ENGLAND

Kocha Arsene Wenger amewapiga mkwara, Tottenham Hotspur, akiwaambia chama lake linakwenda kuufanya Uwanja wa Wembley kuwa uwanja wao wa nyumbani kesho Jumamosi.

Wenger ataiongoza Arsenal yake kwenda kuwavaa mahasimu wao hao wa London, kwenye mchezo wa Ligi Kuu England utakaofanyika hiyo kesho mchana.

Arsenal inashika nafasi ya sita ikiwa pointi nne nyuma ya Spurs na haipaswi kuruhusu kichapo kama inataka kuendelea kuyaweka wazi matumaini ya kuinasa nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Lakini, Wenger amesisitiza Arsenal haijihesabu kama itacheza ugenini kwa wapinzani wao na watauchukulia Wembley kuwa ni uwanja wao wa nyumbani tu.

Wenger alisema: “Ndiyo, tuna rekodi nzuri pale.”

Arsenal haijawahi kupoteza mechi yoyote uwanjani Wembley tangu ilipofungwa kwenye fainali ya Kombe la FA dhidi ya Chelsea mwaka 2009 na tangu hapo imeshinda mara tisa mfululizo kwenye uwanja huo. Kitu kingine anachodai Wenger ni kwamba mastaa wake watakuwa wamepata uwanja wa kucheza kwa kujinafasi.

“Kucheza Wembley haisumbui akili sana kwa sababu tunaamini tunakwenda kuonyesha kiwango chetu bora pale," alisema.

“Mimi sioni kama ni ugenini kwa namna hali ilivyo.”

Mahasimu hao wa Arsenal, Spurs, wamekuwa wakiutumia Wembley kuwa uwanja wao wa nyumbani kwa msimu huu kwenye mechi zao za Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa Ulaya.