Waziri wa Michezo azikurupua Simba, Yanga kujenga viwanja vyao

Dodoma. Waziri wa Habari, Sanaa Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe amezishangaa timu za Yanga na Simba za Tanzania kuwa licha ya umri mrefu lakini hazina viwanja vyao vya michezo.
Dk Mwakyembe ametoa kauli hiyo bungeni wakati anajibu mwongozo wa mbunge wa Mchinga Hamidu Bobale kuhusu timu ya Yanga kuwaachia uwanja timu ya St Louis ya kutoka Shelisheli.
"Yanga wana miaka 83 tangu kuanzishwa kwake na Simba wana miaka 82, ni wakati wa kujitafakari kwani zisiwe na viwanja vyao sasa," amehoji Mwakyembe.
Akizungumzia Uwanja wa Taifa amesema uwanja huo una masharti ambapo hautakiwi kuzidisha michezo mitatu kwa wiki ili uweze kudumu walau miaka kumi tangu matengenezo yake.
Hata hivyo alisema inamshangaza na bado anakuwa na mashaka na watendaji wake kwa kuruhusu michezo mingi ambapo kwa wiki hii uwanja utakuwa umetumika mara tano kitu alichokiita ni 'Uswahili'.
Mwakyembe amesema mchezo wa Yanga na St Louis  kwa kesho itafuatia  mechi ya Simba keshokutwa zote zikitumia uwanja huo.
Bobale alisema timu za Tanzania huwa zinafanyiwa mtimanyongo ziwapo nje ya nchi na kuhoji zababu za TFF kuwapa uwanja wageni ambacho alisema ni hujuma kwa Yanga.
Waziri alipinga hoja hiyo akisema siyo nzuri katika mahusiano na kwamba wanatakiwa kupewa uwanja ili waanze kuuzoea.