Wawakilishi wetu katu msituangushe Afrika

Wachezaji wa klabu ya Zimamoto Zanzibar

Muktasari:

  • Mechi za michuano hiyo mikubwa kwa ngazi za klabu Afrika zilianza tangu jana Ijumaa na zitaendelea kwa wikiendi hii kwa mechi za raundi ya awali.
  • Tanzania kama nchi wanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), nao watakuwa vitani wakiwakilisha na timu zao tatu kati ya nne, kutokana na Azam kusubiri mechi za raundi ya kwanza ndipo ianze kibarua chake Afrika.

MSIMU mpya wa michuano ya kimataifa ya Afrika, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho umeanza upya kwa wawakilishi wa mataifa mbalimbali barani humo wakianza mbio za kuwania mataji ya michuano hiyo.

Mechi za michuano hiyo mikubwa kwa ngazi za klabu Afrika zilianza tangu jana Ijumaa na zitaendelea kwa wikiendi hii kwa mechi za raundi ya awali.

Tanzania kama nchi wanachama wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), nao watakuwa vitani wakiwakilisha na timu zao tatu kati ya nne, kutokana na Azam kusubiri mechi za raundi ya kwanza ndipo ianze kibarua chake Afrika.

Timu ambazo wikiendi hii zitakuwa vitani ni Yanga inayoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika itakayokuwa ugenini kuiwakilisha Tanzania Bara na klabu za KVZ na Zimamoto wanaoiwakilisha Zanzibar watakuwa na kibarua visiwani.

Zimamoto wanaanza kibarua chao leo Jumamosi kwa kuvaana na Ferreviario de Beira ya Msumbiji kwenye Uwanja wa Amaan kabla ya kesho KVZ kuialika dimbani Messenger Ngozi ya Burundi, huku Yanga ikiwa ugenini nchini Comoro.

Yanga itavaana na Ngaya Club de Mbe ya huku katika mechi ambayo haitabiriwi kuwa ngumu kutokana na rekodi zilizopo kwa wawakilishi hao wa Tanzania dhidi ya timu za visiwa hiyo vya Bahari ya Hindi.

Katika mfumo wa sasa michuano hiyo ya Afrika ina mechi chache za mchujo kabla ya klabu kuingia makundini ambapo tofauti za mfumo wa zamani uliohusisha klabu nane, safari hii zitashirikisha timu 16 kuwania kucheza robo fainali na kuendelea mpaka wapatikane mabingwa wa michuano hiyo miwili.

Kwa miaka mingi uwakilishi wa Tanzania bila kujali kama ni Bara ama Zanzibar umekuwa wa aibu kutokana na klabu zetu kuwa wasindikizaji dhidi ya wapinzani wao wa mataifa mengine, wakiwamo walio jirani yetu.

Angalau mwaka jana Yanga ilijitahidi kwa kufika hatua ya makundi ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa klabu za Tanzania katika Kombe la Shirikisho na kurejea rekodi yao ya mwaka 1998 ilipokuwa ya kwanza katika Ligi ya Mabingwa.

Simba wawakilishi wengine wa zamani wa Tanzania miaka ya nyuma waliwahi kucheza makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, pia kufika nusu fainali ya michuano hiyo enzi ikifahamika kama Klabu Bingwa Afrika mwaka 1974 ikacheza pia fainali za Kombe la CAF. Yanga na klabu ya Malindi ya Zanzibar nazo ziliwahi kufika robo fainali za Klabu Bingwa Afrika na Kombe la washindi kwa nyakati tofauti, kitu kinachoonyesha kuwa uwakilishi wa timu zetu katika michuano hiyo ya Afrika ni majanga. Hata hivyo kwa kuwa huu ni mwaka mpya na mambo yake lazima yawe mapya tunaamini wawakilishi wetu hawatatuangusha kwenye mechi zao ili zisonge mbele kwa raundi ya kwanza ambapo watajumuika na Azam.

Azam inayoiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho itaanzia raundi ya kwanza mwezu ujao kwa kuumana na mshindi wa mechi kati ya Orapa United ya Botswana na Mbabane Swallows ya Swaziland.

Wawakilishi wetu wana kila sababu ya kupambana kiume ili zifanye kweli kwenye mechi zao kwa nia ya kurejesha heshima ya soka la Tanzania. Tanzania imekuwa katika hali mbaya sio kwa ngazi za klabu tu, bali hata kwenye uwakilishi wa timu ya taifa na ndio maana haishangazi kuporomoka kwenye viwango ya soka.

Katika orodha iliyotangazwa juzi na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Tanzania imezidi kuporomoka kwenye ubora ikifika nafasi ya 158 kutoka 156 tulipokuwa ndani ya mwezi uliopita wa Januari.

Mwanaspoti linaamini Yanga, KVZ, Zimamoto na hata Azam wamejiandaa vya kutosha kwa nia ya kuliwakilisha vema taifa. Tunaamini wachezaji wa klabu hizo na makocha wao wanajua umuhimu wa kufanya vema katika mechi zao za awali za michuano hiyo ili wasonge mbele na sio kusonga mbele tu, bali wapambane kwa lengo la kujenga heshima ya nchi.Muhimu timu zetu zishuke viwanjani zikiwaheshimu wapinzani wao badala ya kuwadharau na kuona watakuwa na kazi nyepesi, kwa sababu hawajui wenzao wamejiandaa vipi. Hayo yakifanyika na wadau wakaziombea dua njema timu na kuziunga mkono huenda mwaka ukawa poa. Mungu ibariki Tanzania.