Wametikisa kama Mahrez England

Sunday February 11 2018

 

By LONDONENGLAND

SUPASTAA, Riyad Mahrez amerudi kundini na hata jana Jumamosi alitazamiwa kucheza dhidi ya Manchester City huko Etihad.

Winga huyo wa Leicester City alitoweka mazoezini baada ya uhamisho wake wa kwenda Man City kukwama katika dakika za mwisho za kufungwa kwa dirisha la usajili mwezi uliopita. Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Mualgeria huyo kutaka kuihama Leicester City.

Kwenye majira ya kiangazi ya mwaka jana aliwasilisha maombi yake ya kuhama, lakini hakukuwa na klabu iliyokuja na ofa ya maana iliyostahili kunasa huduma yake.

Hata hivyo, staa huyo alirudi mazoezini na bahati njema kwake, amewekwa kwenye orodha ya wachezaji waliotazamiwa kucheza dhidi ya Man City, timu ambayo alitaka kwenda kujiunga nao na kususia mazoezi baada ya mpango huo kukwama.

Hata hivyo, Mahrez si mchezaji wa kwanza aliyeonekana kutaka kuhama au kuweka mazingira ya aina hiyo na namna yalivyopokewa na mashabiki baada ya tukio hilo kama mashabiki wa Foxes walivyomfanyia jana.

Rio Ferdinand – Man United

Rio Ferdinand aliwatibua mashabiki wa Manchester United baada ya kupiga picha kwenye mgahawa akiwa na adui yao. Hiyo ilikuwa mwaka 2005, wakati beki huyo akiwa kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba mpya, lakini usiku mmoja, akiwa na wakala wake, Pini Zahavi alipiga picha na aliyekuwa mkurugenzi mtendaji wa Chelsea, Peter Kenyon kwenye mgahawa mmoja uliopo karibu na Stamford Bridge. Ferdinand alijitetea hakuwa na kitu cha kufanya na mkutano huo haukumhusu ulikuwa wa wakala wake na Kenyon, yeye alikwenda kusalimia tu.Jambo hilo lilimfanya Ferdinand azomewe na mashabiki wa Man United kwenye mechi za kujiandaa na msimu mpya hadi hapo aliposaini mkataba mpya wa miaka minne wenye thamani ya Pauni 90,000 kwa wiki. Rio alizomewa na mashabiki wa Man United waliodhani alikuwa akijichelewesha kusaini mkataba mpya ili ahamie Chelsea.

Carlos Tevez – Man City

Tevez kwanza aliweka bayana dhamira yake ya kuihama Manchester City Desemba 2010, akidai uhusiano wake na mabosi wa klabu hiyo umevunjika na akamtaja kabisa kocha, Roberto Mancini. Maombi yake ya kutaka kuhama yalikataliwa na Man City na hilo liliwatia wasiwasi huenda staa huyo atagomea kucheza tena kwenye timu, hivyo wakampiga mkwara akigoma tu, wanampiga faini. Baadaye akawasilisha maombi ya kuhama na jambo hilo lilimfanya apigwe faini zaidi ya Pauni 750,000 baada ya kugomea kucheza na kuamua kutimkia kwao Argentina, hiyo iliyokuwa 2011. Hat a hivyo, mashabiki hawakumchukia na hata alipoondoka kwenda Juventus walihuzunika sana.

Wayne Rooney – Man United

Mashabiki wa Manchester United walibaki kwenye mshtuko mkubwa mwaka 2010 wakati Wayne Rooney alipotangaza anataka kuihama timu hiyo. Licha ya kwamba hakuandika barua maalumu ya maombi hayo, aliiambia klabu hataki kusaini mkataba mpya na kutaka apewe nafasi ya kwenda kujaribu bahati yake kwingineko. Chelsea walikuwa kwenye mpango wa kumnasa na hilo liliwapa wasiwasi mkubwa mashabiki wa Man United. Manchester City nao walionekana kumtaka fowadi huyo Mwingereza.

Baadaye Rooney alisema tangazo hilo lilikuwa kosa kubwa kuwahi kulifanya kwenye maisha yake kwa sababu lilimfanya apomoroke kiwango chake na kukumbwa na majeruhi ya enka mfululizo. Aliwachukiza mashabiki wa Man United, lakini siku chache akasaini mkataba mpya na miaka mitatu baadaye, akaomba kuondoka tena na Chelsea walimhitaji na kutenga Pauni 40 milioni kumnasa.

Yaya Toure – Man City

Sikia hii, Yaya Toure alitaka kuihama Manchester City kwa sababu haikumpa keki kwenye siku yake ya kuzaliwa. Lakini, hilo liliwekwa tu kuthibitisha Muivory Coast alikuwa amechoka maisha ya Man City na kutaka kuachana na timu hiyo. Katika sherehe za ubingwa wa Ligi Kuu England, iliripotiwa hakuna hata mmoja aliyemtakia heri ya kuzaliwa Toure. Wakala Seluk wake, Dimitry alisema wakati ule: “Yaya amejitolea kila kitu kwenye klabu na hakika ni mchezaji bora kwenye timu, lakini klabu haionekani kumjali. Kilichotokea kwenye siku yake ya kuzaliwa kina maana klabu haimjali. Huo ndio ukweli”.

Wakala huyo alidai anashangaa kwa Yaya kusahaulika wakati ndiye mchezaji aliyewafanya wabebe mataji mawili ya Ligi Kuu England. Siku ya kuzaliwa iliyofuatia, Man City walikumbuka kumnunulia keki Yaya Toure.

Philippe Coutinho – Liverpool

Hatimaye alifanikisha ndoto zake za kwenda kujiunga na Barcelona mwezi uliopita, lakini uhamisho huo aliufukuzia kwa muda kweli kweli.

Kiungo huyo Mbrazili aliwasilisha barua ya kutaka kuhama mwaka jana baada ya kuona anatakiwa na Barcelona, timu ambayo muda wote alikuwa akiitaja kwamba ana ndoto za kwenda kuichezea siku moja. Liverpool waligoma kumuuza wakidai hawataki kupoteza wachezaji wao bora.

Mashabiki kwa nguvu zao zote walionyesha nia na dhamira yao ya kumtaka mchezaji huyo abaki Anfield na ilionekana Liverpool wameshinda vita hiyo kabla ya kufika Januari mwaka huu ambapo Barcelona walirudi na hatimay kumnasa mtu wao.

Barca walilipa Pauni 145 milioni kumsajili Coutinho, mchezaji ambaye bado aliendelea kupendwa na Kop licha ya kuandika barua ya kutaka kuihama Liverpool. Coutinho ataendelea kukumbukwa Anfield.

Steven Gerrard – Liverpool

Mwaka 2005 mashabiki wa Liverpool walikumbwa na jakamoyo baada ya staa wao wa nguvu kutaka kuihama timu hiyo. Mtikisiko uliokuwa mkubwa kuliko huu wa hivi karibuni wa Coutinho kwenda Barcelona.

Kapteni Gerrard alionekana kuvutiwa na mpango wa kwenda kujiunga na Chelsea na wababe hao wa Stamford Bridge walikoleza moto wao kumsajili.

Jose Mourinho wakati huo akiwa Chelsea alivutiwa na kiungo huyo akitaka kumsajili na kumshawishi kwamba akienda hapo atapata nafasi kubwa ya kwenda kubeba mataji, likiwamo la Ligi Kuu England, ambalo ndilo lililokuwa ndoto ya Gerrard. Bosi wa zamani wa Liverpool, Rick Parry, alikiri kiungo huyo alikaribia kabisa kwenda kujiunga na Chelsea.

Lakini, kiungo huyo aliamua kubaki Merseyside kuvaa jezi nyekundu hadi hapo alipoondoka kwenda Marekani na sasa amerudi akiwa kocha wa timu ya watoto huko kwenye akademia.