Wakili wa utetezi akwamisha kesi ya Masogange

Muktasari:

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 26, mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa. Masogange ataanza kujitetea baada ya mahakama kumkuta na kesi ya kujibu baada ya kusikiliza mashahidi watatu wa upande wa mashitaka.

Dar es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya kutumia dawa za kulevya inayomkabili Agnes Gerald maarufu kama ‘Masogange’ umeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kuwaonya upande wa utetezi kwa kushindwa kutoa ushahidi wao kwa mara ya tatu mfululizo.

Upande wa mashtaka, umefikia hatua hiyo baada ya wakili wa utetezi, Nehemia Nkoko kudai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri kuwa wakili mwenzake, Reuben Simwanza ndiye aliandaa mashahidi na kwamba ameshindwa kutokea kwa sababu ni mgonjwa.

Wakili wa Serikali, Constantine Kakula alidai wakati shauri hilo lililofikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Kutokana na hali hiyo, Wakili Nkoko alidai atahakikisha anaandaa mashahidi ili itakapotokea wakili mmoja hayupo, mwengine aendelee na shauri.

Kutokana na hali hiyo, upande wa mashtaka umeomba ahirisho la mwisho kwa sababu kesi ni ya muda mrefu. 

Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 26, mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa.

Masogange ataanza kujitetea baada ya mahakama kumkuta na kesi ya kujibu baada ya kusikiliza mashahidi watatu wa upande wa mashitaka.

Masogange anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 katika maeneo yasiyojulikana ndani ya jiji la Dar es Salaam alitumia dawa za kulevya aina ya Heroin (Diacety Imophine).

Pia anadaiwa kuwa kati ya Februari 7 na 14, 2017 alitumia dawa za kulevya aina ya Oxazepam.