Wadjibouti nao wana mikwara hao

Tuesday February 13 2018

 

By DORIS MALIYAGA

MASHABIKI wa Simba bado wanashangilia ushindi wa timu yao wa mabao 4-0 dhidi ya Gendarmarie ya Djibout, lakini kocha wa kikosi hicho cha maafande wa Djibout, Mvuyekure Issa, amechimba bonge la mkwara.

Kocha huyo ametamba kuwa wanaenda kwao kujipanga na wanaamini kama walipigwa 4-0 ugenini haitakuwa ajabu wao kupindua meza nyumbani kwani wanajua wapi walipokosea.

Kocha huyo Mrundi anayefundisha soka Djibouti kwa zaidi ya miaka 10 sasa, alisema kuna wachezaji waliomtingisha ndani ya Simba kama Shiza Kichuya na John Bocco ‘Adebayor’, lakini atawawekea mikakati ya kuwadhibiti.

“Tumepoteza, lakini tunakwenda kujipanga kwa ajili ya mechi ya marudiano na kama kocha nina imani kabisa ya kurudisha mabao hayo na kushinda kwa sababu huu ni mpira na unadunda,” alisema Mvuyekure.

“Simba ni timu nzuri na kubwa Afrika na kwa sababu vijana wangu hawana uzoefu wowote wa mashindano makubwa kama haya, nilijua tutafungwa mengi hapa lakini kumbe ni woga tu, tunaweza kupindua meza,” alisema Mvuyekule.

Aidha imebainika yale madai yake kwamba walitarajia kupigwa mabao 10 na Simba, zilikuwa mbwembwe tu za kuwapoteza maboya Simba, kwani timu hiyo inayoshikilia nafasi ya nne katika Ligi Daraja la Kwanza nchini kwao, si nyepesi kihivyo.

Katika mechi tisa ilizocheza duru la kwanza, Gendermarie imeshinda mechi tano na kutoa sare mbili ikipoteza michezo miwili.

Katika mabao, imefunga mara 16 na kuruhusu matatu tu wavuni kwake na imekuwa ikigawa dozi za maana kwa wapinzani, tofauti na madai eti imezoea vipigo kwa sababu ina kikosi kilichojaa chipukizi.