Wadau wa michezo waikumbuka Polisi Tanzania

 MOSHI. WADAU mbalimbali wamejitokeza kuisaidia timu ya Polisi Tanzania ambayo imeweka kambi katika Chuo cha Polisi kilichoko mjini hapa kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wake wa hatua ya 16 Bora ya mashindano ya Kombe la FA dhidi ya Singida United.
Polisi Tanzania inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza itasafiri kuifuata Singida United katika mchezo wa raundi ya 16 Bora utakaofanyika kwenye Uwanja wa Namfua kati ya Februari 21 na 25 mwaka huu.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mratibu wa Polisi Tanzania, Robert Munisi, alisema jana kuwa uongozi wa timu hiyo unawashukuru wadau hao kwa sababu misaada waliyotoa itapunguza "makali" ya kambi yao ambayo inaamini ina nafasi ya kuchukua ubingwa wa michuano hiyo.
Munisi aliwataja wadau walioisaidia timu hiyo chakula kuwa ni pamoja na Kampuni ya Le Patio ya jijini Arusha na Family Bakery.
"Tunawashukuru wadau wetu kwa kutupatia mchele, mafuta, sembe huku Family Bakery wao wakitoa mikate kila siku mpaka pale timu yetu itakapoondoka kuelekea Singida kuwafata wenyeji wetu," alisema Munisi.
Katika kuhakikisha timu hiyo inakuwa imara, imejiandaa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya timu ya Kombaini ya Mererani itakayofanyika kwenye Uwanja wa Mirerani mjini humo.