Vigogo Simba watuliza presha

Muktasari:

  • Kwa misimu miwili Simba imekuwa ikiongoza ligi kwa muda,lakini mwisho Yanga inawapiku na kutwaa ubingwa

Sare ya mabao 2-2, iliyopata Simba dhidi ya Mwadui imeifanya timu hiyo kuweweseka katika mbio zao za kusaka ubingwa msimu huu, huku wapinzani wao wakubwa Yanga wakifurahia.

Simba inaongoza Ligi kwa pointi 42, ikiwa mbele kwa pointi tano nyuma ya mabingwa watetezi Yanga wenye pointi 37 na  hivyo kukimbizana kwa kasi kuwania ubingwa msimu huu.

Wekundu wa Msimbazi ambao wamekuwa moto msimu huu kwenye ligi walitegemewa wangeendeleza kasi yao katika mchezo wa juzi dhidi ya Mwadui kwa kuhakikisha wanapata ushindi lakini mambo yakaenda tofauti.

Sare hiyo imewafanya mashabiki wa Yanga kufurahia huku wakitoa maneno mengi kwenye mitandao ya kijamii wakiikebehi Simba kuwa sasa imeanza ugonjwa wake wa msimu uliopita yaani inaongoza ligi kwa muda kisha Yanga inakuja  kuwapita.

Msimu uliopita Simba iliongoza Ligi kwa muda mrefu na kuizidi Yanga kwa pointi nane lakini hadi mzunguko wa kwanza unamalizika Simba ilikuwa ikiongoza kwa pointi 35 na Yanga 33 hivyo kuwa na tofauti ya pointi mbili tu na kuonyesha kuwa Yanga ilifanya kazi kubwa ya kupunguza pengo la pointi huku Simba ikizembea

 Timu hizo ziliendelea kufukuzana katika nafasi hizo mbili za juu lakini Yanga ikaonyesha kuwa si ya kuchezea kwani ilipambana na kuhakikisha inatetea ubingwa wake licha ya kulingana pointi na Simba zote zikiwa na pointi 68 lakini zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Msimu huu pia Simba imeanza vizuri ligi na kuongoza ligi hadi sasa huku Yanga ambayo ilianza ligi kwa kusuasua kadri muda unavyokwenda mabingwa hao watetezi wameanza kurejea katika kasi yao hivyo kuwatia presha wekundu wa Msimbazi ambao wana hofu kuwa yasije ya msimu uliopita yakajirudia.

 Kutokana na maneno mengi kutoka kwa mashabiki wa Yanga,hayakumuacha salama Msemaji wa Simba, Haji Manara ambaye aliibuka na kuandika hivi kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram 

"Baada ya matokeo ya jana mengi yamesemwa moja wapo eti tushayumba,hayo ni maneno yanayotoka kwa watu walewale ambao wanaamini zama ni hizi hizi na Mungu ni wao peke yao,wapuuzeni

"Mwadui imezifunga Singida United na kabla yetu sisi waliwafunga Mtibwa 3-1 kule Shinyanga,wametoka sare na Yanga na Azam tena wakiwa kwao Dar,hizo ndio timu tano kubwa kwenye ligi kwa sasa.Sisi kutoka nao sare kwao kwani nini iwe nongwa tena ugenini?Simba haitatoka mstarini na washabiki wetu tulieni na wajibu wenu ni kuiombea timu na kuisapoti.

"Pia kwa mashabiki wetu muelewe timu yetu bado inaongoza ligi na hatujafungwa bado,haitatokea duniani timu isitoke hata droo.Hata tukimsajili Ronaldo na Messi.Msisahau Mwadui hawa hawa walisababisha Mkwasa atake kupigwa na washabiki wa Yanga baada ya kutoka nao sare hapa jijini"aliandika Manara.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu hiyo,Zacharia Hanspoppe amewatuliza mashabiki  wao na kuwataka  kushusha presha kwani bado wana nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu hivyo hawana haja ya kuwa na wasiwasi.

"Licha ya kwamba tumepata pointi moja dhidi ya Mwadui lakini  mashabiki hawapaswi kuwa na wasiwasi kwani msimu huu tuna kikosi bora hivyo bado tuna nafasi ya kufanya vizuri na kuchukua ubingwa"alisema Hanspoppe.

 Kocha Msaidizi wa Simba,Masoud Djuma alisema udhaifu wa safu yake ya ulinzi ulisababisha wakapata pointi moja kwa kufungwa bao la kizembe na Paul Nonga.

"Udhaifu wa mabeki wangu ulisababisha tukafungwa bao dakika za mwishoni na kutukosesha ushindi,ukweli wameniudhi lakini tunakubali matokeo kwani hatuwezi kushinda kila siku.Tunajipanga kwa mechi zijazo na mashabiki wetu watulie kwani bado tuna nafasi ya ubingwa,"alisema Djuma