Vibaoni United, Wanawake Live waibuka kidedea Uchumi Cup

Monday February 12 2018

 

By Rajabu Athumani

Handeni. Vibaoni United imetwaa ubingwa wa kwanza wa mashindano ya Uchumi Cu kwa kuifunga Kurugenzi FC kwa mabao 3-0 katika fainali iliyofanyika kwenye Uwanja wa Kigoda, wilayani Handeni mkoani Tanga.

Vibaoni United ilipata mabao yake katika dakika ya 5 kipindi cha kwanza na mawili katika kipindi cha pili katika fainali hiyo ya kwanza ya mashindano hayo.

Nahodha wa Vibaoni United, Omari Nyambulo alisema mechi ilikuwa ngumu kutokana na timu hizo kuchez kwa kukamiana, lakini wamefanikiwa kutwaa ubingwa. “Mechi ilikuwa ngumu maana sisi wote ni watoto wa mjini, lakini tunashukuru tumewafunga 3-0 wakajipange upya kwa shindano yajayo,”alisema Nyambulo.

Naye nahodha wa Kurugenzi Fc, Mwaliko Machele alisema anakubali matokeo na mchezo haukuwa na kasoro yoyote pia kuomba kuanzishwa kwa michuano mingine ili kutoa fursa kwa vijana kuonyesha vipaji vyao.

Mdhamini na muasisi wa mashindano hayo Mkuu wa wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe alisema wamepata timu itakayopewa jina na wahusika kwaajili ya kuanza mapambano rasmi.

Alisema wataandaa mashindano mengine kwaajili ya kuendeleza vipaji vilivyoonekana katika mashindano kwani wamegundua wananchi wa Handeni wanapenda michezo ila fursa ndio hakuna.

Katika netiboli Wanawake Live imetwaa ubingwa kwa kuifunga Kivesa Sekondari kwa magoli 44-14, katika fainali ya mchezo huo.