Urafiki wa Willian, Mourinho kuvunjia Old Trafford

Muktasari:

Miamba hiyo inapigania kumaliza katika nne bora ya Ligi Kuu England msimu huu

London, England. Kiungo wa Chelsea, Willian ni rafiki mkubwa wa kocha wake wa zamani Jose Mourinho, lakini kesho atauweka kando urafiki wao wakati atakapokutana na Manchester United katika mchezo wa Ligi Kuu England.

Kiungo huyo Mbrazil alijiunga na Chelsea mwaka 2013, ikiwa chini ya Mourinho, ambaye alitimuliwa miaka miwili iliyopita kabla ya baadaye kujiunga na Man United mwaka 2016.

Willian mwenye miaka 29, amefunga mabao manne na kutegeneza mabao saba katika mechi 26, alizochezea Chelsea msimu huu chini ya Antonio Conte ambaye timu yake imeachwa kwa pointi tatu na Manchester United inayoshika nafasi ya pili.

"Mourinho ni rafiki yangu. Nimekuwa na wakati mzuri chini yake, lakini mimi ni mchezaji wa Chelsea nay eye sasa ni kocha wa Manchester United," alisema Willian.

"Itakuwa mechi ngumu. Kwa ujumla ni kazi ngumu kucheza katika Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa kwa pamoja. Nafikiri tutabaki katika kiwango chetu hiki wakati tutakaposhuka Old Trafford na michezo mingine."

Baada ya mchezo wa Old Trafford, Chelsea itawafuata Manchester City na Crystal Palace kabla ya kurudiana na Barcelona hapo Machi 14.