Ukame wa mabao nje ya Dar wamwandama Okwi

Muktasari:

Mshambuliaji huyo hajafunga bao lolote nje ya Dar es Salaam tangu kuanza wa msimu huu

Kagera. Mshambuliaji Emmanuel Okwi ameendeleza rekodi yake mbovu ya kutopachika bao katika mechi za ugenini baada ya kushindwa kufunga katika ushindi wa mabao 2-0 iliyopata Simba dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Kagera.

Katika mchezo huo mabao ya Simba yalifungwa na kiungo Said Ndemla na John Bocco na kuhakikishia vinara hao wa Ligi Kuu kulipa kisasi cha msimu uliopita.

Okwi aliyeingia kwenye mchezo wa jana akiwa na kumbukumbu ya kutoka kupachika mabao mawili katika mchezo uliopita dhidi ya Singida United alijikuta akiwekwa mfukoni na Juma Nyosso  ambaye hakumpa nafasi ya kupumua.

Nyosso kwa mara ya kwanza alikutana na Bocco tangu alipokumbana na adhabu ya kufungiwa miaka miwili, Septemba 30, 2015, kwa kosa la kumdhalilisha mshambuliaji huyo, alimuwekea ulinzi mkali Okwi kuanzia dakika ya kwanza hadi kipyenga cha mwisho kilipopulizwa jambo lililomfanya Okwi atoke patupu.

Kutokana na historia ya Nyosso na Bocco, wengi walitegemea kuona vita ya uwanjani baina ya wawili hao, lakini mwisho wa siku beki huyo aliamua kumfungia kazi Okwi huku jukumu la kumdhibiti Bocco likiwa mikononi mwa beki mwingine wa zamani wa Simba, Mohammed Fakhi.

 

Beki huyo wa zamani wa timu za Simba, Ashanti na Mbeya City alionekana kumpania Okwi asifurukute kwenye mchezo huo hali iliyopelekea ajikute akipewa kadi ya njano dakika za mwanzoni za kipindi cha kwanza kwa kumchezea rafu mshambuliaji huyo ambaye amecheza michezo mitatu ugenini bila kufunga bao dhidi ya timu za Mbao, Stand United na Mbeya City.

Bao la kwanza lilifungwa na Said Ndemla lilitokana na uzembe uliofanywa na mabeki wa Kagera Sugar kushindwa kuundosha mpira kutoka miguu mwa Shiza Kichuya ambaye alimpasia mfungaji aliyeunganisha kwa shuti kali la mguu wa kulia. Awali John Bocco alinasa mpira uliorudishwa na Atupele Green wa Kagera Sugar na kumpasia Okwi ambaye alipiga pasi ya kichwa kwa Kichuya.

Wakati wakishangazwa na bao hilo, mlinzi wa kushoto wa Kagera Sugar, Adeyum Ahmed alijikuta akifanya makosa mengine kwa kushindwa kumdhibiti Shomari Kapombe ambaye krosi yake iliunganishwa na Bocco aliyefunga bao la pili.

Hata hivyo mchezo huo ulitawaliwa na ubabe kwa wachezaji wa timu zote mbili hali iliyomlazimisha refa Shomari Lawi kutoka Kigoma kuwazawadia kadi za njano Nyosso, Fakhi, George Kavila, Bocco na Juuko Murshid kwa faulo walizozicheza.

Kapombe alisema nashukuru Mungu, familia yangu na watu wote waliokuwa na mimi katika kipindi cha miezi sita niliyokuwa nje lakini si kitu rahisi kwangu kucheza mechi ya kwanza nikiwa na timu yangu mpya na kuanza vizuri kwa kucheza vizuri," .
"Naendelea kujipanga katika mechi zijazo ili kupata nafasi kama hii na kuisaidia Simba kama matumaini yao kwangu yalivyokuwa wakati wananisajili," alisema Kapombe ambaye hajacheza hata mechi moja ya ligi tangu aliposajiliwa na Simba mwanzoni mwa msimu,” alisema Kapombe.