Uchumi Cup yaleta amshaamsha Handeni

Handeni. Mwanzilishi wa Mashindano ya Uchumi Cup Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Godwin Gondwe ametamba kuunda timu ambayo itapambana na timu kubwa za Mkoa wa Tanga  pamoja na timu nyingine.

Gondwe amesema hayo jana Alhamisi wakati akikabidhi jezi kwa timu mbili zilizofanya vizuri kwenye nusu fainali za Kurugenzi FC na Mtazamo FC na kusema kuwa ataunda timu ambayo ana uhakika itaamsha ari ya ushabiki kwa wananchi wa Handeni.

Alisema kuwa baada ya mashindano hayo, wataunda timu moja ambayo itakuwa na wachezaji watakaoweza kupambana na timu nyingine na kuleta ushindi Handeni.

Mratibu wa mashindano hayo, Baraka Nkatura alisema Uchumi Cup imeweza kuamsha hamasa kwa michezo mingine ambapo vipaji vingine pia vimeonekana kujitokeza.

Alisema wachezaji wa mpira wa pete nao wamejitokeza na wanafanya vuzuri hivyo  kuleta hamasa kwa waanzilishi kuona umuhimu wa kuzisaidia timu hizo.

Nahodha wa timu ya Mtazamo FC, Athumani Madanga alisema kuanzishwa kwa mashindano hayo kumesaidia timu zao kuonekana na kufanya vizuri hivyo kuwa na nafasi ya kupanda daraja kama watasaidiwa vifaa vya mazoezi.

Katika mpambano wa timu hizo zilitoka suluhi katika dakika 90 hivyo muamuzi kuwapa nafasi ya kupiga penalti ambapo Mtazamo ilitolewa kwa mikwaju mitano ya penalti.