Uchaguzi ngumi waota mbawa, uongozi wavunjwa

Muktasari:

BMT imeunda kamati ya muda ya miezi mitatu ya kusimamia ndondi za riadhaa

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Mohammed Kiganja ameuvunja uongozi wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa (BFT), kwa kuwaengua Katibu Mkuu Makore Mashaga na makamu wa rais, Lukelo Wililo katika kamati ya muda ya shirikisho hilo.

Katibu Mkuu wa BMT, Kiganja aliwaondoa vigogo hao na baadhi ya wajumbe wa kamati tendaji katika hatua ya usaili kwa kile alichodai hawastahili kuendelea kuongoza Shirikisho hilo kwenye uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike leo mkoani Dodoma.

"Uchaguzi wa BFT hautofanyika na badala yake naunda kamati ya watu sita ambayo itasimamia shirikisho kwa kushirikiana na BMT kwa miezi mitatu kabla ya kuitisha uchaguzi upya," alisema Kiganja.

Aliwataja wajumbe hao ni Rais wa BFT, Mutta Lwakatare atakayekuwa mwenyekiti, Yona Kivela, Samwel Tumwa, Mohammed Abubakar na Aisha Abunuas.

"Kamati hii itaratibu ushiriki wa timu ya Taifa ya ngumi kwa ajili ya michezo ya madola, pia mkutano mkuu na itapaswa kuitisha uchaguzi mkuu ndani ya miezi mitatu kuanzia leo," alisema Kiganja na kuongeza.

"BMT tunahitaji viongozi watendaji hivyo hataweza kuwavumilia watu ambao si watendaji katika vyama vya michezo na hii haitaishia kwenye ngumi, itafanyika kwenye michezo yote yenye viongozi wasiowajibika."