Tunasubiri ushindani mkubwa duru la pili VPL

Muktasari:

  • Ni wazi kwamba timu zilipata muda wa kutosha kufanya marekebisho ya kutosha katika vikosi vyao baada ya kupewa muda huo wa mwezi mmoja ili kufanya usajili. Ikumbukwe kuwa ligi zimesimama tangu Novemba 11 hivyo hata muda wa kujiandaa vizuri na duru la pili uliokuwepo.

USAJILI wa timu za Ligi Kuu na zile za Ligi Daraja la Kwanza nchini unafungwa leo Alhamisi ili kuruhusu duru la pili la ligi hizo kuendelea keshokutwa Jumamosi baada ya mapumziko ya zaidi ya mwezi mmoja.

Ni wazi kwamba timu zilipata muda wa kutosha kufanya marekebisho ya kutosha katika vikosi vyao baada ya kupewa muda huo wa mwezi mmoja ili kufanya usajili. Ikumbukwe kuwa ligi zimesimama tangu Novemba 11 hivyo hata muda wa kujiandaa vizuri na duru la pili uliokuwepo.

Tuliona katika kipindi hicho timu kama Azam, Simba, Yanga, Kagera Sugar na Stand United zikifanya usajili uliotikisa ili kuziba nafasi ambazo zilionyesha mianya katika duru la kwanza la Ligi Kuu.

Azam walifanya usajili wa nyota wawili wa kigeni ambao ni Samuel Afful na Yahya Mohammed huku pia mshambuliaji wao mwingine, Mghana Enock Agyei akijiunga na timu hiyo licha ya kwamba atalazimika kusubiri hadi mwezi Januari ili aweze kuitumikia timu hiyo kwa kuwa bado hajatimiza miaka 18.

Simba imemwongeza kipa Mghana, Daniel Agyei, kiungo James Kotei kutoka Ghana pia pamoja na mshambuliaji Pastory Athanas kutoka Stand United ya Shinyanga wakati Yanga imewasajili kiungo Mzambia, Justine Zulu pamoja na mshambuliaji Emanuel Martin kutoka JKU ya Zanzibar.

Timu nyingine kama Kagera Sugar imewaongeza Ame Ali na kipa mkongwe Juma Kaseja huku Mtibwa Sugar ikipandisha wachezaji kutoka timu yao ya vijana. Mtibwa haikutaka kusajili mchezaji yoyote katika dirisha hili dogo kwa imani kuwa timu yao imekamilika na mapungufu yaliyokuwepo siyo makubwa.

Mbali na usajili, timu kadhaa pia zimefanya mabadiliko ya makocha kwa kuwaondoa wale waliokuwepo mwanzo na kuleta wapya. Simba kwa upande wake haijafukuza kocha bali imemwongeza Iddi Salim kama kocha mpya wa makipa ili kuwaongezea makali Vincent Angban, Manyika Peter na Agyei.

Yanga ilifanya mabadiliko ya benchi lake la ufundi mapema kwa kumpandisha aliyekuwa Kocha mkuu, Hans Van Pluijm kuwa Mkurugenzi wa Ufundi huku Mzambia, George Lwandamina akipewa shavu kama kocha mkuu.

Timu nyingine kama Ndanda iliamua pia kumpandisha Hamim Mawazo kuwa Mkurugenzi wa ufundi huku wakiwa mbioni kumtangaza kocha mpya. Stand United imempa ajira Hemed Morocco aliyekuwa kocha msaidizi wa Taifa Stars wakati Mwadui imempa timu Ali Bushiri aliyetokea timu ya KMKM ya Zanzibar.

JKT Ruvu iliachana na aliyekuwa kocha wao Malale Hamsini na kumpa timu kocha wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Bakari Shime wakati ambapo Ruvu Shooting walimchukua Malale na kuachana na Selemani Mtingwe aliyekuwa na timu hiyo katika duru la kwanza.

Prisons ya Mbeya nayo imefanya mabadiliko pia ya benchi lake la ufundi kwa kuachana na Meja Mstaafu, Abdul Mingange na kuleta kocha mpya.

Mabadiliko haya makubwa yaliyofanyika kwa timu za Ligi Kuu tunaamini kuwa yalizingatia mahitaji ya kiufundi na yatakuwa na tija kwa timu hizo katika duru la pili.

Tunatarajia kuona mechi za duru la pili zikiwa na msisimko zaidi na matokeo yasiyotabirika tofauti na duru la kwanza ambapo baadhi ya mechi zilionekana wazi kuwa hazikuwa kiushindani. Mfano katika duru la kwanza timu kama Majimaji ya Songea iliweza kwenda mechi saba bila kupata walau sare moja.

Tungependa kuona wachezaji wapya wakizibeba timu kama Azam ambazo hazikuwa pia na mfululizo wa matokeo mazuri katika duru la kwanza. Timu kama Simba na Yanga tunategemea pia zitaendelea kuwa na kasi zaidi ambayo walionesha katika ile duru ya kwanza.

Hii ndiyo mantiki halisi ya timu kupewa muda wa kufanya maboresho ya vikosi vyao na kujiandaa kwa ajili ya duru la pili, hivyo ni lazima kuwepo na tofauti ya ufanisi wa timu ukilinganisha na ule wa duru la kwanza.

Kwa upande mwingine, mashabiki nao wamekaa mkao wa kula, wanataka kuona soka safi likitandazwa kwa ajili ya burudani kwa wale wanaoingia uwanjani au kuangalia kupitia runinga.