Tshishimbi afunika taifa

Sunday February 11 2018

 

By CHARLES ABEL

YANGA imeanza vizuri kampeni yake ya mechi za kimataifa baada ya jana Jumamosi jioni kuichapa St Louis ya Shelisheli bao 1-0 katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo ni kama haujawapa furaha kubwa Wanayanga kwani waliamini timu yao itashinda mabao mengi kutokana na wapinzani wao kuonekana kama timu ya kawaida, lakini kiungo wake, Papy Kabamba Tshishimbi alifunika mbaya.

Kiwango cha Tshishimbi kilikuwa cha juu kuliko namna Yanga ilivyocheza katika pambano hilo, huku nyota wengine wa timu hiyo wakichemsha.

Makala haya yanaangazia kwa undani namna nyota wa Yanga walivyokiwasha kwa St Louis.

Ramadhan Kabwili-6

Alikuwa likizo muda mrefu kutokana na wapinzani wao kutolisogelea lango la Yanga mara kwa mara ingawa kuna wakati alifanikiwa kuokoa hatari ndogo ndogo golini kwake.

Aliwapanga na kuwakumbusha majukumu mabeki wake kila wakati hali iliyofanya wapinzani wasilete madhara makubwa.

Hassan Kessy-7

Yanga walimtumia zaidi Kessy kuanzisha mashambulizi kutokana na kasi yake ambayo ilionekana kuwa mwiba kwa Gervais Waye-Hive na Steve Henriette waliokuwa wanacheza upande wa kushoto wa St. Louis.

Hata hivyo, hakutumia vyema udhaifu wa wapinzani kwani alipiga krosi nyingi ambazo hazikufikia walengwa. Kazi kubwa zaidi ilikuwa kusababisha penalti baada ya kuangushwa na mabeki wa St. Louis, hata hivyo, Obrey Chirwa kama kawaida yake aliikosa dakika ya 24.

Gadiel Michael-6

Hakuwa na jukumu kubwa katika kulinda na mara kwa mara alisogea katika eneo la St. Louis kama mbinu ya kujaribu kuwarudisha wachezaji waliokuwa wakicheza upande wa kulia wa timu pinzani kurudi nyuma zaidi jirani na lango lao.

Hata hivyo, hakuweza kupiga krosi za mara kwa mara kutokana na Yanga kuutumia zaidi upande wa kulia.

Said Juma ‘Makapu’-5

Alichezeshwa kama mlinzi wa kati sambamba na Kelvin Yondani na kwa kiasi kikubwa alifanikiwa kumdhibiti mshambuliaji Elijah Tamboo ambaye St. Louis walimsimamisha mbele.

Hata hivyo, Makapu hakuwa na maamuzi ya haraka pindi awapo na mpira na mara kwa mara alipiga pasi za pembeni ambazo ziliichelewesha Yanga kusogea mbele.

Kelvin Yondani-7

Alitimiza vyema majukumu ya ulinzi kwa kushirikiana na Makapu kumdhibiti Tamboo, pia mara kwa mara alipanda mbele kusaidia mashambulizi jambo lililoifanya Yanga iwe na idadi kubwa ya wachezaji kwenye lango la timu pinzani.

Kuna wakati alijaribu mwenyewe kusaka bao kwa kupiga mashuti ambayo hata hivyo yalitoka nje ya lango ama kudakwa na kipa wa Louis.

Papii Kabamba Tshishimbi-8

Kutokana na idadi kubwa ya wachezaji ambao St. Louis iliwajaza kwenye safu ya kiungo, Tshishimbi alijikuta akifanya kazi kubwa ya kuilinda safu yake ya ulinzi pamoja na kuchezesha timu.

Alikuwa kinara wa kupora mipira kutoka kwa wapinzani wao, pia aliziba mianya ambayo ingewafanya St. Louis kutengeneza nafasi za mabao.

Ibrahim Ajibu-6

Alihaha huku na kule kutafuta na kusambaza mipira akitumia vyema uwezo wake wa kupiga pasi sahihi zinazofikia walengwa kwa wakati.

Alionekana mwiba kwa mabeki wa St. Louis kutokana na namna alivyokuwa anachezesha timu hali iliyosababisha Yanga ipate idadi kubwa ya faulo ambazo hata hivyo hazikutumiwa vizuri.

Alikosa mabao mawili ya wazi dakika ya 34 na ile ya 60 ambayo pengine yangeifanya Yanga iondoke na ushindi mnono na haikushangaza kuona akitolewa dakika ya 65 na nafasi yake kuchukuliwa na Juma Mahadhi.

Rafael Daud-5

Hakuwa amechangamka na kasi yake pindi awapo na mpira ilikuwa ndogo hali iliyowafanya St. Louis kujipanga mapema pindi alipokuwa na mpira na kuwapa urahisi wa kuokoa mashambulizi.

Alionekana kuchoka mapema mwanzoni mwa kipindi cha pili hali iliyompa kazi kubwa Tshishimbi ambaye alijikuta akizungukwa na idadi kubwa ya viungo wa St. Louis.

Obrey Chirwa-7

Kipindi cha kwanza hakuonyesha sana makeke yake kutokana na kutopigiwa aina ya pasi ambazo amekuwa akizitumia vyema kuwasumbua mabeki wa timu pinzani.

Kasi yake ilionekana kurudi kipindi cha pili hali iliyowalazimu St. Louis kutumia mabeki wawili ili kumdhibiti. Hakuwa na bahati ya kufunga kwenye mechi ya jana kwani alikosa penati dakika ya 24 lakini pia alikosa bao la wazi kipindi cha pili.

Pius Buswita-6

Alipambana uwanja mzima kuhakikisha anapata mipira na kuitawanya kwa wachezaji wenzake lakini aliangushwa na kasi ndogo ya Yanga pindi ilipokuwa ikielekea langoni mwa timu pinzani.

Alikuwa mahiri katika kuunganisha mipira ya krosi lakini mara kwa mara vichwa alivyopiga vilitoka nje.

Dakika ya 87 alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Yusuph Mhilu baada ya kiungo huyo mshambuliaji kuonekana amechoka.

Emmanuel Martin-4

Hakuwa na kasi na alionekana kutoka mchezoni katika dakika za mwanzoni za kipindi cha kwanza tofauti na ilivyozoeleka.

Alipiga idadi kubwa ya krosi ambazo zilitoka nje na mara kwa mara alipoteza pasi jambo ambalo liliwasaidia wapinzani wao kupoteza muda na kujipanga.

Walioingia

Juma Mahadhi-7.5

Kuingia kwake dakika ya 65 kuliiamsha Yanga ambayo ilianza kupeleka mashambulizi makali langoni mwa St. Louis.

Alitumia muda usiozidi dakika moja tangu alipoingia kuchukua nafasi ya Ajibu, kuifungia Yanga bao na pengine angeingia mapemawangepata ushindi mnono.

Geoffrey Mwashiuya 6

Aliongeza uhai katika safu ya ushambuliaji ya Yanga kutokana na kasi yake na kumpa wakati mgumu beki wa kulia wa St. Louis Jean Paul Aglae.

Hata hivyo alionyesha udhaifu katika kupiga krosi na pasi za mwisho ambazo nyingi zilinaswa na walinzi wa St. Louis.

Yusuph Mhilu 2

Aliingia dakika ya 87 kuchukua nafasi ya Pius Buswita katika kile kilichoonekana kama mbinu ya Yanga kutafuta mabao zaidi kwa dakika chache zilizosalia.

Hata hivyo hakuweza kuonyesha madhara kwani hakuweza kupata nafasi ya kuchezeshwa na wenzake jambo lililomfanya asionyeshe makeke.