Totti: Salah? Wala hanishangazi

LIVERPOOL, ENGLAND. Mkongwe wa AS Roma, Francesco Totti amesema hashangazwi na kiwango cha soka linalochezwa na mshambuliaji Mohamed Salah huko Liverpool msimu huu.

Totti alicheza na Salah alipokuwa kwenye kikosi cha AS Roma na alisema hivi kuhusu staa huyo wa Misri: “Soka analocheza kwa sasa, nadhani amekuwa mmoja wa wanasoka bora duniani na ninachoamini ataendelea kuwa bora siku zinavyozidi kusonga.

“Namfahamu vizuri rafiki yangu mzimu na anapenda kupandisha kiwango bora cha soka lake ili kuwa mchezaji bora. Anapenda kufanya mambo yake kuwa mazuri, anafanya sana mazoezi, anajituma na anasikiliza anachoambiwa na makocha, ndiyo maana unamwona alivyo bora kwa sasa. Nadhani bado kuna kiwango cha juu zaidi cha soka kitafuata kutoka kwake."

Katika maelezo yake, Totti anaamini pia Liverpool ya msimu huu inayonolewa na Mjerumani, Jurgen Klopp itabeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya ambapo itakuwa mara ya sita kwa upande wao.

“Salah ni mmoja wachezaji wale wanaoweza kuleta mambo tofauti kwenye mechi kubwa, alisema Totti na kuongeza.

“Ndiyo maana sioni kwanini Liverpool wasitajwe kwenye mbio za ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu. Sawa kuna timu nzuri zilizokamilika, lakini unakuwa na mchezaji kama Salah, unapaswa kuamini chochote kinawezekana."