Timu hizi zinapaswa kuwa na namba ya simu ya Antonio Conte

Muktasari:

  • Conte ni kocha mwenye uzoefu mkubwa na huduma yake ni jambo litakalokuwa na maana kubwa kwenye klabu hizo tano za Ulaya, ambazo hakika zitapaswa kuwa na simu ya Mtaliano huyo kumdaka haraka haraka kama bilionea Roman Abramovich ataamua kumfungulia mlango wa kutokea huko Stamford Bridge kutokana na Chelsea kufanya ovyo siku za karibuni.

MAMBO si mambo kwa Mtaliano Antonio Conte huko Chelsea, lakini jambo hilo litazizindua klabu kibao za Ulaya zinazofuatilia kwa karibu suala lake. Hakika kuna klabu kibao za Ulaya zitakuwa zinahangaika kwa sasa kutafuta simu ya kocha huyo kuwa nayo ili kama atafutwa kazi huko Stamford Bridge wamkimbilie fasta kupata huduma yake.

Conte ni kocha mwenye uzoefu mkubwa na huduma yake ni jambo litakalokuwa na maana kubwa kwenye klabu hizo tano za Ulaya, ambazo hakika zitapaswa kuwa na simu ya Mtaliano huyo kumdaka haraka haraka kama bilionea Roman Abramovich ataamua kumfungulia mlango wa kutokea huko Stamford Bridge kutokana na Chelsea kufanya ovyo siku za karibuni.

Arsenal

Staa wa zamani wa Arsenal, Paul Merson ametoa pendekezo la klabu yake kuhakikisha wanamchukua Conte kwenda kurithi mikoba ya Arsene Wenger kwenye kikosi hicho cha Emirates.

Arsenal imekuwa ikirudi nyuma kwa siku za karibuni wakiwa chini ya Wenger, hivyo wanahitaji kufanya mabadiliko na kwenye hilo, Conte atawafaa zaidi kwenye wakati huu wa kufanya mapinduzi.

Kitakuwa kitu kizuri pia kwa Conte mwenyewe kwenda Arsenal mahali ambako suala la kubadilisha makocha mara kwa mara si kitu kinachopewa nafasi tofauti na huko aliko kwa sasa Stamford Bridge.

Real Madrid

Zinedine Zidane amekuwa hana nyakati nzuri kwa sasa huko Real Madrid licha ya kuanza maisha yake ya ukocha kwenye timu hiyo kwa kasi kubwa na nzuri.

Kocha huyo Mfaransa alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya mara mbili katika misimu yake miwili ya kwanza huko Bernabeu, lakini mambo ya msimu huu yanaonekana kuwa magumu zaidi na pengine anaweza kukutwa na makubwa.

Hakuna ubishi kama Conte mwenye uzoefu zaidi akipatikana, basi itakuwa jambo zuri kama Real Madrid wataamua kumchukua na kumbadili Zidane. Kama Zidane ataondoshwa, hakuna ubishi, Conte atawafaa kama naye pia ataonyeshwa mlango wa kutokea huko Stamford Bridge.

PSG

Hakuna, ubishi PSG wanafanya vizuri sana msimu huu baada ya kuwa na huduma za mastaa makini kama Neymar, Kylian Mbappe, Edinson Cavani na wengineo.

Hawaonekani kuwa na tishio lolote katika kuubeba ubingwa wa Ligue 1, lakini changamoto inayowakabili ni kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambako kocha wao wa sasa Unai Emery haonekani kuwa na mbinu za kuweza kulibeba taji hilo. Kocha huyo Mhispaniola pengine alifanya vizuri alikotoka Sevilla, lakini PSG ni mahali tofauti kutokana na timu hiyo kwa sasa kufanya usajili wa wachezaji wenye majina makubwa. Kutokana na hilo, Conte anaweza kuwa mtu sahihi kabisa kwenda kubadilisha kiwango cha PSG.

Inter Milan

Ni kitu unachokitarajia klabu za Italia lazima zitapigana vikumbo kuwania huduma ya kocha Conte hasa kutokana na kazi ile aliyofanya Juventus alipokuwa kocha wa timu hiyo.

Inter inahitaji kubadilisha mipango yao ya kufanya vizuri kwenye soka na Kocha Luciano Spalletti alionekana kufanya mambo makubwa, lakini upepo kwa sasa umebadilika tofauti na ilivyokuwa mwanzo wa msimu.

Hivyo, Inter watakuwa kwenye mikono salama zaidi kama watakwenda kuwa chini ya Kocha Conte ambaye anaweza kushawishika kurejea kwenye Serie A kama ataamua kurudi nyumbani.

AC Milan

Hii ni nafasi nzuri kwa AC Milan kuamka upya baada ya kuonekana kupoteza kwenye soka lao. Kama Kocha Conte atapatikana atakapoachiwa na Chelsea basi hiyo itakuwa nafasi nzuri kwa AC Milan kuchangamkia fursa ya kumchukua ili kwenda kuwawekea mambo yao sawa.

Kocha huyo wa zamani wa Juventus atakuwa na msaada mzuri kwa AC Milan kuliko hata kocha wao wa sasa, Gennaro Gattuso, ambaye kimsingi hana uzoefu wa kutosha wa kuinoa klabu kubwa na yenye historia kubwa kama hiyo. Kama Conte atafutwa kazi huko Chelsea siku za karibuni, Rossoneri watakuwa wamefanya jambo zuri kabisa kama watamtwangia simu ili aende akawaokoe.