Timu 10 za vijana kushiriki mashindano ya kuogelea

Jumla ya timu 10 zimethibitisha kushiriki katika mashindano ya taifa ya kuogelea kwa vijana wa umri kuanzia miaka saba mpaka 14 yaliyopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Katibu Mkuu wa klabu ya Dar Swim Club (DSC), Inviolata Itatiro alizitaja klabu hizo kuwa ni Bluefins, Arusha Swim Club, Shule ya Kimataifa ya Moshi, Mwanza Swim Club na Champion Rise.

Vilabu vingine kwa mujibu wa Inviolata ni Taliss, Hopac, Wahoo ya Zanzibar, Kennedy House, Shule ya Kimataifa ya Morogoro na wenyeji, DSC.

Inviolata alisema kuwa wameandaa mashindano hayo  kwa lengo la kuendeleza mchezo wa kuogelea nchini na hasa waogeleaji chipukizi ambao ni nguzo ya nchi katika mashindano yajayo ya kimataifa.

Alisema kuwa wanatarajia waogeleaji zaidi ya 200 katika mashindano hayo yamepangwa kuanza Januari 26 na kumalizika Januari 27.

“Maandalizi yanaendelea na kwa sasa tunaomba wadhamini watusaidie kufanikisha mashindano haya, ni mashindano ya vijana wadogo ambao wanahitaji kuona kila kitu kinakuwa sawa, ni muhimu kupata msaada kutoka kwa wadau na makampuni,” alisema Inviolata.

Alisema kuwa klabu yake inaandaa mashindano haya kwa mara ya pili na mafanikio yameanza kuonekana kwani kuna waogeleaji wengi chipukizi wameanza kuwa tishio katika mashindano ya Taifa.

Alifafanua kuwa wamepewa kibali na Chama cha Kuogelea Tanzania (TSA) kufanya mashindano hayo  ambayo awali yalikuwa ya ngazi ya vilabu kabla ya kupandishwa kuwa ya kitaifa.