Tanzania yasuasua ushiriki Chipukizi Cup

Muktasari:

Mashindano hayo yanashirikisha timu za vijana kutoka katika nchi mbalimbali za Afrika

Arusha. Jumla ya timu 85 za vijana wadogo chini ya miaka saba hadi 20 kutoka Ghana, Kenya, Uganda na Tanzania wanatarajia kushiriki mashindano yajulikanayo kama ‘Chipukizi Cup’ yanayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Desemba 13 hadi 17 mwaka huu.

Mashindano hayo yaliyoandaliwa na taasisi ya kukuza vipaji vya michezo ‘future stars’ kwa kushirikiana na chama cha soka wilaya ya Arusha yatashirikisha timu katika vitengo mbalimbali ikiwemo chini ya miaka saba, tisa, 11, 13, 15, 17 na 20.

Mashindano hayo yatatanguliwa na semina ya awali ya michezo yatakayotolewa na kocha kutoka nchini Denmark, Daniel Locovic ambae mbali na kufundisha kozi hiyo pia anakuja kuibua na kusaka vipaji vya vijana wadogo ili kuwakuza zaidi.

Mkurugenzi wa taasisi ya Future Stars, Alfred Altael alisema mashindano hayo ya Chipukizi Cup yanatimiza miaka nane sasa tangu kuanzishwa kwake.

“Tumepata muitikio mkubwa hasa Kenya wameleta jumla ya timu 54 tofauti na wenyeji Tanzania wenye timu 26, Uganda na Zanzibar wakileta timu nne kila mmoja ambapo Ghana walithibitisha kushiriki lakini bado timu haijawasili nchini tunasubiri hadi saa 24 kuanzia leo,”

 Mwenyekiti wa chama cha soka wilaya ya Arusha, Omary Walii alionyesha kusikitishwa na ushiriki wa wenyeji Tanzania kuzidiwa  idadi na majirani zao Kenya.

 “Ndio maana wenzetu wanazidi kupanda viwango vya Fifa sisi tunazidi kushuka  na kupanda, lakini kwa nafasi hiyo hiyo ya zaidi ya 100, hii inatokana na hatuna dhamira ya kweli ya kuendeleza soka letu wenyewe hassa kwa kuanzia chini kwa hawa vijana wadogo”