Tambwe, Kakolanya amsha amsha Yanga

Amissi Tambwe (pichani) akifanya mazoezi na wenzake jana kwenye Uwanja wa Uhuru. PICHA:MICHAEL MATEMANGA

Muktasari:

  • Tambwe hajaonekana uwanjani tangu mwishoni mwa mwezi uliopita kwenye kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Mbao

YANGA inalazimika kupambana na hali yake katika mechi tatu zijazo baada ya staa wake, Obrey Chirwa, kufungiwa kucheza michezo mitatu kwa kukutwa na makosa ya utovu wa nidhamu katika mechi yao na Prisons iliyochezwa Novemba, mwaka jana.

Hata hivyo, mastaa wake wengine Amissi Tambwe na Beno Kakolanya, ni kama wamepunguza machungu hayo baada ya jana Jumatatu kurejea kuongeza nguvu katika kikosi cha timu hiyo kinachojiandaa na mchezo dhidi ya Mwadui kesho Jumatano kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Tambwe hajaonekana uwanjani tangu mwishoni mwa mwezi uliopita kwenye kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Mbao, huku Kakolanya akirejea klabuni hapo baada ya awali kujitoa akishinikiza kulipwa fedha zake za usajili.

Kurejea kwa Tambwe aliyekuwa majeruhi kumeongeza hamasa na ushindani katika safu ya ushambuliaji ya timu hiyo ambayo kwa sasa imeshikwa na Yohana Mkomola na Juma Mahadhi. Kakolanya anatarajiwa pia kuanza kumpa ushindani kipa Youthe Rostand, ambaye mashabiki wa timu hiyo tayari wameanza kupata wasiwasi na kiwango chake.

Yanga itaivaa Mwadui katika pambano ambalo vijana wa Jangwani watakuwa na kazi ya kuhakikisha wanapata ushindi ili kufuta machozi ya kipigo walichopewa katika mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu dhidi ya Mbao.

Watetezi hao walipigwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na kuchangia kuongeza pengo lao na watani zao Simba waliopo kileleni, hivyo ni ushindi pekee ambao utarejesha furaha ya mashabiki wa timu hiyo.

Yanga ipo nafasi ya tano na alama zake 21 baada ya kuteremshwa na Mtibwa Sugar walioshinda wikiendi iliyopita dhidi ya Lipuli na kama itapata ushindi kesho itaifanya ifikishe pointi 24 na kurejea katika nafasi ya tatu kwa uwiano mzuri wa mabao ikiwazidi Wakata Miwa yenye alama kama hizo baada ya kucheza mechi 13.

NI YANGA SIO SIMBA

Katika hatua nyingine mashabiki mbalimbali wa Yanga kupitia mitandao ya kijamii walimpa ubani wa Sh 3 milioni, Kocha George Lwandamina aliyefiwa na mwanaye hivi karibuni nchini Zambia.

Katika toleo letu la jana iliandikwa kimakosa kwa kutaja mashabiki wa Simba, ila ukweli ni kwamba waliotoa fedha na pole hiyo kwa Lwandamina ni wanachana na mashabiki wa Jangwani.