Taifa Stars ya kuivaa Algeria hii hapa

Dar es Salaam. Kocha msaidizi wa Taifa Stars, Hemed Morocco ametangaza kikosi cha wachezaji 23 watakaocheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Algeria na DRC Congo.

Vijana hao wa Salum Mayanga wataanza kwa kucheza ugenini dhidi ya Algeria Machi 22, 2018 na siku tano baadaye watareja nchini kuwakabili DR Congo Machi 27, 2018 Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Taifa Stars inategemea kuingia kambini Machi 18 na kuondoka Machi 19 kuelekea nchini Algeria kwa mchezo huo wa kirafiki ukaochezwa Machi 22.

Algeria kwa sasa ipo nafasi 60 katika orodha ya viwango vya ubora wa Fifa wakati Tanzania ikiwa nafasi ya 146 iwapo Tanzania itashinda itapanda zaidi katika orodha hiyo ya Fifa.

Baada ya mechi hiyo siku Machi 27, Stars itarejea nchini kujiandaa na mechi nyingine ngumu zaidi dhidi ya DR Congo iliyo nafasi ya 39, katika orodha ya ubora wa Fifa.

Taifa Stars na DR Congo wamekutana mara tano tangu 1995, mara mbili katika mechi za mashindano na mara tatu katika michezo ya kirafiki.

Tanzania imeshinda mechi mara mbili, sare moja na kufungwa mechi mbili mara ya mwisho zilipokutana Februari 23, 2012 timu hizo zilitoka suluhu.

Kikosi hicho kitaundwa na makipa, Aishi Manula (Simba), Ramadhani Kabwili (Yanga), Abdulraham Mohammed (JKU).

Mabeki ni Shomari Kapombe (Simba),Hassan Kessy (Yanga),Gadiel Michael (Yanga),Kelvin Yondani (Yanga), Abdi Banda (Baroka), Erasto Nyoni (Simba).

Viungo ni Hamisi Abdallah (Sony Sugar), Mudathir Yahya (Singida United), Said Ndemla (Simba), Faisal Salum (JKU), Abdulazizi Makame (Taifa Jang'ombe), Farid Mussa (CD Tenerife), Ibrahim Ajib (Yanga), Shiza Kichuya (Simba) Mohammed Issa (Mtibwa Sugar) na Thomas Ulimwengu.

Washambuliaji ni Mbwana Samatta (KRC Genk), Saimon Msuva (Difaa El Jadida), John Bocco (Simba), Zayd Yahya (Azam).