TFF yajazwa manoti na Fifa

Muktasari:

Hizo ni fedha za maendeleo na uendeshaji kutoka Fifa ambazo Tanzania ilifungiwa kuzipata tangu mwaka 2015.


Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inatarajia kupata Dola 1 milioni (Sh 2.24 Bilioni) kutoka Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) katika miradi ya maendeleo ya mchezo wa soka nchini.

Hizo ni fedha za maendeleo na uendeshaji kutoka Fifa ambazo Tanzania ilifungiwa kuzipata tangu mwaka 2015.

Fifa ilisitisha kutoa fedha hizo kwa Tanzania kutokana na  changamoto za uongozi uliopita ulioongozwa na Jamal Malinzi ambaye hivi sasa yuko mahabusu akikabiliwa na kesi ya utakatishaji fedha.

Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Harrison Mwakyembe alisema kutokana na changamoto ya uongozi uliopita TFF ilizuiwa kupata fedha za maendeleo na uendeshaji kutoka Fifa tangu mwaka 2015 ambapo kila mwaka nchi wanachama hupata dola 250,000.

"Tumemthibitishia rais wa Fifa, Gianni Infantino kuwa uongozi wa sasa wa TFF umeanza vizuri na umeweza kuaminiwa kwa fedha hizo hivyo Serikali itaendelea na utaratibu wake  wa kutoingilia uamuzi ya TFF na vyombo vyake vya ndani, lakini macho yetu hatutayafumba wala masikio hatutayaziba kwa pamba kwani ndio wajibu wa Serikali na viongozi wa Fifa wamebariki,"alisema Mwakyembe.

Alisema chini ya Rais Infantino ameongeza fedha za maendeleo na uendeshaji kutoka dola 250,000 hadi  dola 1,250000 sawa na sh 2.79 bilionihivyo kuwataka TFF kuwa makini kwa kufanya kazi yao vizuri ikiwemo kuwasilisha mahesabu yaliyo safi na kufanya miradi inayoonekana ili kuepuka kuzuiwa tena kupokea fedha hizo.  

Naye Rais wa TFF, Wallace Karia alisema Infantino amewahakikishia licha ya fedha hizo kutokuja tangu 2015 ziko salama makao makuu ya Fifa Uswisi.

"Ametuhakikishia kuwa fedha ziko salama na tunasubiri siku watakayoamua kuanza kutupa tena hivyo tunaamini watatoa zote za kuanzia 2015 hadi mwaka huu"alisema Karia 

Mashindano ya Vijana ya  Afcon

Mwakyembe alimshukuru Rais wa Caf, Ahmad Ahmad kuwaruhusu mashindano ya Afrika ya vijana chini ya miaka 17 (Afcon) kufanyika mkoa wa Dar es Salaam  pekee.

"Tulimshukuru rais wa Caf, Ahmad kwa uteuzi wa Tanzania kuendesha mashindano ya Afcon ya vijana, lakini sana kwa kuturuhusu mashindano kufanyika Dar es Salaam na si mikoa miwili kama tulivyopanga mwanzo kwani uamuazi huo utatupunguzia mzigo wa gharama,” alisema Mwakyembe.