TFF iharakishe kutoa maamuzi tata kuepuka lawama

Muktasari:

Ligi hiyo ilisimama kwa muda huo ili kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2017 iliyomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita na Azam FC kuibuka mabingwa.

LIGI Kuu ya Vodacom, inazidi kuchanja mbuga ambapo utamu wake umerejea upya baada ya kusimama kwa muda wa wiki mbili.

Ligi hiyo ilisimama kwa muda huo ili kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2017 iliyomalizika mwishoni mwa wiki iliyopita na Azam FC kuibuka mabingwa.

Kwa sasa ligi ipo duru la pili ambalo ni hatua ya lala salama, ambapo klabu 16 shiriki zipo kwenye mbio za kuwania ubingwa na nyingine kupambana kuepuka kushuka daraja, hivyo kuifanya ligi kuwa na ushindani mkubwa zaidi.

Ndio kipindi ambapo lawama na malalamiko huwa yanaongezeka maradufu, hasa juu ya waamuzi sambamba na hisia za upangaji wa matokeo.

Sio katika Ligi Kuu tu, bali hata katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na Daraja la Pili (SDL) ambazo nazo zinaelekea kwenye ngwe ya mwisho kabla ya kufunga msimu huu.

Kama ilivyo kwenye VPL, hata kwenye FDL na SDL kuna timu zinawania kupanda daraja na zipo zinazopambana kuepuka kushuka daraja, hivyo kufanya ngwe hii kuwa yenye ushindani mkubwa na kipindi cha kusikia lawama kila kona.

Kutokana na hali hiyo ni wazi wasimamizi wa Ligi Bodi ya Ligi na Kamati ya Mashindano kuwa makini ili kuhakikisha mechi hizi za lala salama zinachezeshwa vema na kutoa matokeo yasiyo na shaka ili kupunguza lawama hizo.

Kuwepo kwa umakini pia kutasaidia mwishoni mwa ligi kupatikana washindi halali na hata timu zitakazoshuka daraja zitaridhika kwa kuamini uzembe wao na kushindwa kujipanga mapema ndiko kulikosababisha zivune kile ilichopanda.

Mbali na umakini pia Shirikisho la Soka (TFF) na kamati zake zinapaswa kufanya haraka kutoa maamuzi ya kesi ama mashtaka yaliyowasilishwa mezani kuhusu masuala ya ligi hiyo, ili kusaidia kuepuka ulalamishi mbele ya safari.

Tunafahamu yapo malalamiko na kesi zilizofunguliwa au kuwasilishwa TFF na ambazo zinapaswa kusikilizwa na kutolewa maamuzi mapema, ili kuweka mambo sawa.

Kuchelewesha kusikilizwa kwa mashauri hayo yanayohusiana na mwenendo wa ligi kunaweza kuzua mzozo, iwapo maamuzi yatakuja kutolewa wakati ligi ikielekea mwishoni.

Kwa mfano yapo malalamiko na rufaa dhidi ya wachezaji na timu shiriki katika ligi hizo, TFF haipaswi kunyamazia na kusubiri ligi hizo zikielekea ukingoni ndipo zije na maamuzi mwishoni.

Maamuzi ambayo wakati mwingine huenda yakaathiri misimamo ya ligi hizo, ndio maana tunatoa rai kwa TFF na kamati zake kuchangamkia kesi zilizopo mezani mwao na kutoa maamuzi sasa kabla ligi hizo hazijasonga mbele.

Kwa mfano Yanga imeikatia rufaa African Lyon kwa kumchezesha aliyekuwa straika wa Mbao, Venance Ludovick ambaye hata klabu yake ya Mbao nayo inalalamika kuwa hajasajiliwa kihalali, kiasi cha kuruhusiwa kucheza, lakini mpaka sasa hakusikiki kitu.

Klabu ya Mshikamano FC inadaiwa kulalamika kufanyiwa vurugu walipoumana na Lipuli Iringa na mifano ya malalamiko hayo ni lazima yatolewa maamuzi mapema ili kumaliza utata kabla ligi haijafikia mwishoni.

Kadhalika ni lazima TFF na kamati zake ziwe na jicho la ziada katika kufuatilia mechi hizi za lala salama hasa katika ligi za FDL na SDL, kwani huko ndiko kwenye matatizo makubwa kwa kuwa hila za kupandisha timu daraja zimekithiri. Hilo limekuwa likiathiri sana na kushusha hadhi ya ligi zetu hivyo kusababisha soka letu kuendelea kudidimia badala ya kukua.

Tunaamini TFF na kamati zake zina masikio sikivu na jicho la kufuatilia kwa makini ligi hizo hatua hii ya lala salama, ili kuwe na mwisho mzuri wa ligi zetu na kama bingwa ama zilizopanda daraja au kushuka kila moja ikubali na kuridhika na kuzipa fursa klabu hizo na nyingine kujipanga kwa msimu ujao. Umefika wakati sasa malalamiko ya klabu yapatiwe ufumbuzi kwa haraka.