TFF epukeni aibu hii ndani ya Ligi Kuu Bara 2016-2017

Muktasari:

Ni mechi inayosubiriwa kwa hamu kuwa na mashabiki wa soka ambao, wangependa kutaka kuona timu hizo zimejiandaaje kwa msimu huu ambao ufunguzi wake utaanza Jumamosi ya wiki hii.

PAZIA la msimu mpya wa Ligi Kuu Bara linatarajiwa kufunguliwa rasmi kesho Jumatano kwa pambano la Ngao ya Hisani, kati ya mabingwa wa msimu uliopita, Yanga na washindi wa pili wa msimu huo na Kombe la FA, Azam FC.

Ni mechi inayosubiriwa kwa hamu kuwa na mashabiki wa soka ambao, wangependa kutaka kuona timu hizo zimejiandaaje kwa msimu huu ambao ufunguzi wake utaanza Jumamosi ya wiki hii.

Mwanaspoti ikizitakia timu hizo na nyingine 14 zitakazoshiriki ligi ya msimu huu maandalizi mema ya msimu mpya, kuna jambo ambalo kama wadau wa soka tunapaswa kulikumbusha Shirikisho la Soka Tanzania, TFF.

Katika ligi iliyopita na hata msimu mmoja nyuma, TFF imekuwa ikijisahau na kufanya mambo ambayo sio tu yamekuwa yakikera mashabiki na klabu shiriki za Ligi Kuu, bali yamekuwa yakiitia doa na kulichafua shirikisho hilo.

Panga pangua ya ratiba ya ligi hiyo kila baada ya muda mfupi ni dosari kubwa kwa TFF na lazima wabadilike. Waendeshe mambo yao kisasa badala ya kuishi kwa mazoea jambo ambalo limekuwa likishusha hadhi ya ligi yetu.

Ingawa tayari panga pangua ya msimu huu imeanza mapema hata kabla ligi haijaanza kwa sababu mbalimbali zilizotolewa hivi karibuni, ikiwemo suala la kutokamilika kwa Uwanja wa Kaitaba, Kagera, lakini tunadhani haitatokea tena.

Ni aibu kubwa ratiba ya ligi inapanguliwa kama mechi za mchangani, mbaya zaidi ni kwamba sababu za kufanya jambo hilo huwa hazina mashiko na zinaonekana kuwa nyepesi sana na nyingine zinaweza kuzuilika.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi alilalamika sana kwenye hafla ya kuwazawadia tuzo washindi wa Ligi Kuu msimu uliopita kuwa, amekuwa akiandamwa na kuandikwa vibaya na wanahabari.

Alitumia muda mwingi kuwanyooshea vidole baadhi ya wanahabari tena kwa majina.

Sio jambo baya, mradi ametoa dukuduku lake, lakini kama hataweza kudhibiti tatizo la panga pangua ya ratiba ya ligi atarajie kuandamwa zaidi.

Ingawa jambo hili halikuanzia kwenye utawala wake tu, panga pangua ilikuwapo tangu enzi za Leodger Tenga, lakini wengi waliamini utawala wa Malinzi ungetatua tatizo hilo kwa kujifunza kutokana na makosa na mtangulizi wake.

Ndio maana watu wamekuwa wakimshutumu kwa kuona bado hata katika utawala wake umeendelea na kasumba hiyo na mbaya zaidi mechi zinaahirishwa ili tu kuruhusu timu iende kushiriki bonanza nje ya nchi. Hii haikubaliki aslan.

Hivyo kwa nia njema ya kutaka kuona ligi ya msimu huu inakuwa tamu zaidi, ndio maana Mwanaspoti inalikumbusha shirikisho hilo na viongozi wake wakuu kuwa, waepuke aibu hii ndani ya msimu huu.

Kama tunapenda kuiga mazuri ya mataifa mengine katika uendeshaji wa ligi, vipi kwa hili la kupanga ratiba isiyoyumba linashindikana? Tubadilike. Panga pangua ifanywe pale inapolazimika tena sababu ikiwa ni majanga ya kiasili yanapotokea kama ambavyo mara nyingi tumeona katika ligi za wenzetu hasa Ulaya.

Sio kiongozi anaenda kuoa, tunaamua kusimamisha ligi ili kupisha harusi ifanyike. Hii haitakuwa ligi kuu labda ni mechi za ndondo ambazo hata hivyo ndani ya Sports Extra Ndondo Cup haijawahi kushuhudiwa kituko kama hicho.

Kituko cha kupangua ratiba kienyeji, ili kupisha mambo yasiyo na tija kwa michuano husika. Tunaamini panga pangua iliyofanywa mapema ni mwanzo na mwisho, hakutakuwa na kitu kama hicho tena hadi mwisho wa msimu. Labda!