TFF, TPLB wanapaswa kuepuka aibu za aina hii

Rais  wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi.

Muktasari:

  • Kitu cha kushukuru ni kwamba kwa sasa Ligi Kuu inaenda mapumziko, lakini tunadhani kama ingekuwa ikiendelea, tungeshuhudia madudu zaidi kwani ni kama TFF na Bodi la Ligi (TPLB) wameshindwa kuwajibika kama wasimamizi. Karibu duru zima la kwanza la ligi hiyo panga pangua imekuwa ya kawaida mno kiasi cha kukera, huku sababu za kufanyika kwa mambo hayo yakiwa hayana mashiko kabisa wala kueleweka kwa wadau wa soka na klabu kwa ujumla.

        RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi aliwahi kunukuliwa na gazeti hili kuwa, panga pangua ya Ligi Kuu Bara haiepukiki na wala haitakuja kuisha mara moja kutokana na mazingira ya nchi yetu ilivyo. Inawezekana alichokisema Malinzi ni sahihi, lakini bado kuna panga pangua nyingine za Ligi Kuu ni kama kujitia aibu tu kwa shirikisho hilo na watendaji wake.

Kitu cha kushukuru ni kwamba kwa sasa Ligi Kuu inaenda mapumziko, lakini tunadhani kama ingekuwa ikiendelea, tungeshuhudia madudu zaidi kwani ni kama TFF na Bodi la Ligi (TPLB) wameshindwa kuwajibika kama wasimamizi. Karibu duru zima la kwanza la ligi hiyo panga pangua imekuwa ya kawaida mno kiasi cha kukera, huku sababu za kufanyika kwa mambo hayo yakiwa hayana mashiko kabisa wala kueleweka kwa wadau wa soka na klabu kwa ujumla.

Wasimamizi wa ligi wamekuwa ni kama watu wanaofanya kazi zao kwa mazoea tu na sio weledi, ndio maana unaona mechi za viporo vya Simba, Yanga na Azam zilivyokuwa zikibadilishwa kila mara kama wasimamizi hao wamekurupushwa usingizini. Tangu mwanzoni mwa Oktoba ilifahamika kuwa mechi hizo zingechezwa kati ya Novemba 9-12, baada ya awali kushindwa kuichezwa katika tarehe iliyopangwa kwa sababu ya mchezo wa kirafiki ya kimataifa ya Taifa Stars dhidi ya Ethiopia ambayo hata hivyo haikuwapo.

Lakini wasimamizi hao wamekuwa wakibadilisha siku kadri wanavyojisikia na hasa kwa timu za Simba na Yanga. Tarehe ya mchezo kati ya Azam iliyopangwa kuumana na Mwadui mjini Shinyanga ilibaki kama ilivyo Novemba 9, yaani jana, lakini mechi ya Simba dhidi ya Prisons na ile ya Yanga dhidi ya Ruvu Shooting ilikuwa kizungumkuti.

Mechi ya Simba awali ilipangwa kuchezwa Novemba 12, ikarudishwa Novemba 10 kabla ya kuamuriwa ichezwe jana, wakati ile ya Yanga awali ratiba ilionyesha ingechezwa kesho Ijumaa, ilirudishwa mpaka jana Jumatano, lakini yakatolewa maamuzi mengine kuwa, ichezwe leo Alhamisi.

TFF ilitoa taarifa juzi jioni kuwa mechi hizo tatu za viporo zingechezwa siku moja ya jana Jumatano, ili kupisha muungiliano na mipango ya timu ya taifa, Taifa Stars inayotarajiwa kuwahi Harare, Zimbabwe kuumana na wenyeji wao katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa unaochezwa Jumapili hii.

Unaweza kujiuliza, TFF ilikuwa haijui kama kuna mchezo huo wa kimataifa unaotambuliwa na kalenda ya Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) ama ilipopanga mechi ya Yanga na Ruvu kuchezwa Jumatano hawakujua kama timu ya Ruvu ilikuwa ipo Kagera kuumana na wenyeji wao hivyo ilikuwa mtihani kwao?

Ilikuwaje waliipanga mechi ya Simba na Prisons ichezwe Alhamisi kabla ya kubadili ichezwe jana, wakati walikuwa wanafahamu timu zote zimecheza mechi Jumapili hazikuwa umbali mrefu kama ilivyokuwa kwa Ruvu Shooting? Lakini baada ya tishio la Ruvu kutishia kususia mechi hiyo ndio wakaona aibu na kukubali kuisogeza mbele kutoka jana na kuwa leo Alhamisi. Hapa ndipo tunaposema kuwa aibu nyingine dhidi ya TFF na TPLB zinaepukika kama watendaji wake wataacha kufanya kazi kwa mazoea badala yake watumie weledi na uzoefu wao ndani ya mamlaka hizo zinazosimamia Ligi Kuu Bara.

Panga pangua na ratiba zisizo rafiki kwa timu ndogo zinachangia kuifanya ligi yetu kuwa ya ovyo na hata kupunguza mvuto wake, jambo ambalo linachangia pia kuwaacha solemba mashabiki wanaopenda kwenda uwanjani. Bahati ni kwamba duru la kwanza zimeshamalizika na mechi zilizokuwa zikipangwa na kupanguliwa ni za viporo, la sivyo ilikuwa aibu kubwa kwa TFF na TPLB.

Ndio maana Mwanaspoti linasisitiza kuwa, wakati ligi ikienda mapumziko, TFF na TPLB zitumie nafasi hii kujitathmini na kurekebisha dosari.