Stand United yapania kuvunja mwiko Mbeya

Muktasari:

  • Miamba hiyo ya Shinyanga kwa sasa ipo nafasi ya 12 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara

 Stand United haijawahi kupata ushindi kwenye Uwanja wa Sokoine tangu imependa Ligi Kuu, lakini imeweka wazi wanataka kuvunja mwiko huo kesho, Jumapili watakapoikabili Mbeya City mjini Mbeya.

Chama hilo la Wana lenye maskani yake mjini Shinyanga imecheza mechi nane kwenye Uwanja wa Sokoine lakini hawajawahi kuondoka na pointi tatu.

Uwanja huo unatumiwa na Tanzania Prison na Mbeya City umekuwa mwiba kwa Stand United katika michezo yake ya Ligi Kuu.  

Kocha Msaidizi wa Stand United, Agustino Malindi alisema kesho ndio itakuwa mwisho wa wao kuondoka Mbeya bila kupata pointi tatu.

Alisema wanajua mchezo wao na Mbeya City utakuwa mgumu lakini wao wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na ushindi kama walivyofanya kwa Singida United.

“Hatujawahi kupata pointi tatu hapa Mbeya  tangu tumepanda Ligi Kuu, lakini sasa tumejipanga na kwa mara ya kwanza tutapata ushindi ,”alisema Malindi.

Hata hivyo kocha huyo alisema kipa wao Frank Muwonge sasa amerejea kikosi baada ya kuugua ghafla wakati wa mchezo wao na Singida United.

“Kipa Muwonge amerejea kikosi alikuwa akisumbuliwa na tumbo ambalo lilimfanya aweze kulazwa hospitali kule Singida lakini sasa yupo fiti,” alisema Kkocha huyo.