Stand United yaota nne bora

Monday February 12 2018

 

By Masoud Masasi

Mwanza. Baada  ya kuwatandika Singida United kwa bao 1-0, Stand United imesema sasa watapambana wahakikishe wanamaliza katika nafasi nne za juu za Ligi Kuu Bara.

Chama hilo la Wana jana liliwashangaza mashabiki wake baada ya kupata ushindi huo ugenini kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida kwa bao pekee la Sixtus Sabilo alilofunga dakika ya 84.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Athumani Bilali “Bilo” alisema sasa wamejipanga kila mechi kupata matokeo mazuri ambayo yatawafanya wamalize Ligi kuanzia nafasi ya nne na kuendelea.

“Ligi bado mbichi hivyo kama tukipambana na kuhakikisha kila mchezo tunapata matokeo mazuri  basi tutaweza kumaliza tukiwa katika nafasi nne za juu ”alisema Bilo.

 “Ligi Kuu msimu huu haina nyumbani wala ugenini anayeshinda ni yule alijiandaa ndani ya uwanja jambo linalotupa nguvu ya kupambana kwani hapa hakuna upendeleo, ” alisema kocha huyo.

Stand United ipo nafasi ya 11 ikiwa na pointi 19 katika msimamo wa Ligi Kuu huku Singida United ikiwa ya nne na pointi zake 33.