Zamu ya Nani leo FA!

Muktasari:

Yanga, waliifunga Ashanti mabao 4-1, huku Simba, ikiibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Polisi Dar, Prisons waliifunga Mbeya Warriors 2-1, na Toto imewafunga Mwadui kwa penati 5-4.

MECHI za Kombe la FA, zinaendelea leo Jumanne kwenye viwanja mbalimbali tayari klabu za ligi kuu zikiwemo Simba na Yanga, zimeshaweka heshima dhidi ya timu za daraja la kwanza.

Yanga, waliifunga Ashanti mabao 4-1, huku Simba, ikiibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Polisi Dar, Prisons waliifunga Mbeya Warriors 2-1, na Toto imewafunga Mwadui kwa penati 5-4.

Mechi za leo kwa timu zinazoshiriki ligi kuu ni Mtibwa Sugar dhidi ya Polisi Moro, JKT Ruvu itakuwa mgeni wa Kurugenzi, Mbeya City dhidi ya Kabela City na nyingine ni Madini na Panone za daraja la kwanza.

Kipa wa Mtibwa, Said Mohamed alisema hawaibezi Polisi Moro, lakini watapambana kuonyesha ukomavu wao kwenye soka .

“Ikumbukwe Polisi Moro, ilikuwa inashiriki ligi kuu inapambana kurejea tena, hivyo watakuwa na mazoezi ya kutosha lakini tumejipanga kuhakikisha tunafuata mkondo wa Simba na Yanga, zimekuwa na mwanzo mzuri,” alisema.

Naye Kocha wa JKT Ruvu, Bakari Shime, alisema kikosi chake kipo vizuri kuwakabili Kurugenzi: “Ni mechi ngumu ila siku zote kitu cha kuwania wengi kinahitaji kujiamini, kujituma na umakini, tumejipanga, tunajua tutakutana na ushindani wa kutosha,”alisisitiza

Naye kiungo wa Mbeya City, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ alisema: “Ili ufanikiwe muhimu kuonyesha ubora kwa aliye juu yako na ndicho kinachofanyika zinapokutana timu za ligi kuu na daraja la kwanza ila naamini tutaibuka na ushindi,’’ alisema

Mechi za kesho Jumatano ni Singida United na Kagera Sugar na African Lyon ya Dar es Salaam, itakuwa mwenyeji wa Mshikamano.