Yanga yahamishia machinjio Mwanza

Winga wa Yanga, Simon Msuva (kushoto) akitafuta mbinu za kumtoka mchezaji wa Zanaco, Taonga Mbembya wakati wa mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliofanyika kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini Lusaka jana. Timu hizo zilitoka suluhu. Picha na Gift Macha

Muktasari:

  • Iko hivi;  Mchezo dhidi ya Ngaya  ya Comoro Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 5-1 ugenini lakini ilipokuja Taifa mambo yakageuka na kulazimishwa sare ya bao 1-1,  Matokeo ya APR dhidi ya Yanga msimu uliopita ambao ugenini Yanga ilishinda kwa mabao 2-1 lakini sare kama hiyo ya Ngaya ikatokea Taifa.

YANGA inakusudia kuhamishia mechi zake za kimataifa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kwa madai kwamba makelele ya Simba yanawazingua wachezaji wao Jijini Dar es Salaam.

Yanga wanadai kwamba Wachezaji wao wamekuwa hawana uhuru wanapokuwa Uwanja wa Taifa lakini wanapokuwa ugenini wanachezaji kiwango cha juu zaidi.

Ilichoshtuka Yanga ni kwamba inapotumia uwanja wa Taifa katika mechi zao za nyumbani hasa kimataifa kuna mkono wa Simba katika kuwapa motisha wapinzani wao mbalimbali na kujikuta wakijiweka katika wakati mgumu.

Iko hivi;  Mchezo dhidi ya Ngaya  ya Comoro Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 5-1 ugenini lakini ilipokuja Taifa mambo yakageuka na kulazimishwa sare ya bao 1-1,  Matokeo ya APR dhidi ya Yanga msimu uliopita ambao ugenini Yanga ilishinda kwa mabao 2-1 lakini sare kama hiyo ya Ngaya ikatokea Taifa.

Wiki moja iliyopita ikaambulia sare ya bao 1-1 dhidi ya Zanaco iliyowaondoa katika Ligi ya Mabingwa msimu huu baada ya pia kulazimishwa suluhu juzi ugenini.

Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Samuel Lukumay ambaye aliiongoza Yanga kwenda Zambia pamoja na staa wa timu hiyo, Simon Msuva wamesisitiza kwamba sasa imetosha ni bora Yanga ihamie Mwanza mashabiki wao wataifuata hukohuko.

Lukumay ambaye ni miongoni mwa vigogo wenye ushawishi ndani ya Yanga kwasasa, alisema ; “Unajua hili nimelichunguza sana hapa, Taifa, hapana Simba wanahusika nitawasilisha ombi maalumu kwa wenzangu, tujadiliane. Angalia Mpira ambao Yanga imecheza hapa Zambia, kama tungecheza hivi nyumbani mambo yangekuwa tofauti ila tunapokuwa nyumbani wachezaji wanakuwa wazito kitu ambacho kimekuwa kikitushangaza.

“Mashabiki wa Yanga wamekuja Zambia kwa mabasi ni umbali mrefu kwa mapenzi ya timu yao sidhani kama watashindwa kwenda Mwanza,” alisema huku akiungwa mkono na Msuva.

“Kuna mambo mengi ambayo yanatukwaza tunapocheza nyumbani hatuna raha kucheza nyumbani hata Simba nao wanahusika katika hilo,” alisema Msuva ambaye awali ilizushwa kwamba Zanaco wanamtaka kabla ya kuja kubainika kwamba walikuwa wakiichezea Yanga akili ili wawaondoe.

Kwa mujibu wa Alfred Lucas ambaye ni msemaji wa Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF), viwanja vinavyokidhi viwango vya CAF kwa Bara ni Taifa na Chamazi pekee.

Aliongeza kwamba Kirumba haukidhi viwango vyumbani na nyasi za kuchezea hivyo timu yoyote itakayotaka kuutumia ni lazima ukarabatiwe kwa kiwango hicho na CAF waje wajiridhishe.

Miaka ya nyuma Yanga iliwahi kuhamishia mechi zake uwanja huo, lakini haikuwa sababu ya Simba, ni kutokana na Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) kukarabatiwa.

Yanga imekata tiketi ya Kombe la Shirikisho Afrika na wanasubiri ‘kapu’ kupata mpinzani kabla ya kuingia hatua ya makundi.