Yanga yafanya umafia

Muktasari:

Waarabu hao wanadai wamepata habari kwa watu wao kwamba Yanga itawachezesha majira ya saa 8 badala ya saa 10 jioni.

LICHA ya kwamba CAF haijawaambia rasmi kwamba mechi ni Aprili 8, MC Alger wameanza kulialia kwamba Yanga imepanga kuwafanyia umafia Taifa kwa kuwachezesha kwenye jua kali la nyuzi joto 40.

Waarabu hao wanadai wamepata habari kwa watu wao kwamba Yanga itawachezesha majira ya saa 8 badala ya saa 10 jioni.

Omar Ghrib ambaye ni Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, alidai jana kwamba wanachotaka kuwafanyia Yanga ni kama walichokutana nacho Ghana na DR Congo.

Kwenye mechi za awali za Kombe la Shirikisho, MC Alger ilifungwa na Bechem United ya Ghana mabao 2-0 ugenini na iliporudi nyumbani ikawafunga mabao 4-1 na kuwaondosha.

Katika mechi dhidi ya Renaissance ya Congo, nyumbani walishinda mabao 2-0 lakini walipokwenda Kinshasa wakafungwa mabao 2-1 na wakafuzu.

Omar anadai kwamba Yanga wanapanga kufanya hivyo ili kupata matokeo mazuri nyumbani kwavile Algeria hali ya hewa ni nyuzi joto 19 wakati wa mchana ambayo ni baridi ya wastani. Jioni inapungua mpaka 12 ambayo ni baridi ya kuvaa koti au sweta.

Kwa Dar es Salaam katika siku za hivikaribuni, mchana majira ambayo Yanga wanataka mechi hiyo ichezwe, kunakuwa na joto kali la nyuzi 32.

“Hatujapokea tarehe rasmi ya mechi kutoka CAF ila tunajua walichopanga kufanya Yanga na tunajua kwamba mechi itachezwa mchana kama zinavyofanyika mechi zote za Afrika,”alisema kiongozi huyo huku Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwassa akisisitiza watulie bado wanaendelea na mipango.

Anasema kwamba timu hiyo itakaa Tanzania kwa siku tatu na watatua nchini Aprili 5. Hatahivyo, kama Yanga watakubaliana kucheza mechi hiyo mapema watalazimika kujipanga kimazoezi kwani mechi nyingi za Ligi wamekuwa wakicheza majira ya saa 10 jioni na mazoezi wanafanya asubuhi kabla jua halijawa kali.

Kuhusu kucheza juani, kocha wa Mbeya Warriors inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza, Mrage Kabange alisema; “Sioni kama itakuwa na faida kwa Yanga kucheza dhidi ya Waarabu Juani kwani inaweza kuwaathiri wao pia. Watambue kuwa Dar es Salaam sasa kuna joto kali kwani hata mechi zote zinazofanyika muda wa kawaida ambao ni saa 10 unaona kabisa jinsi joto linavyokuwa kali sasa wakicheza mchana si wanatafuta matatizo.

“Cha muhimu ni kufanya maandalizi, wajiandae kisaikolojia kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo,”alisisitiza kocha huyo mwenye kadi ya uanachama wa Simba.