Yanga yabinafsisha kombe bwana

Muktasari:

Zaidi ya miaka kumi iliyopita Yanga haijawahi kufungwa na Toto iwe ndani au nje ya Dar es Salam. Kama Yanga watalibeba kombe hilo leo watakuwa wamekabidhiwa rasmi kikanuni na Shirikisho la Soka la Tanzania litapaswa kutengeneza kombe lingine.

KAMA rekodi zitabaki jinsi zilivyo kabla giza halijaingia leo Jumanne, Yanga itakuwa bingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mara ya tatu mfululizo.

Zaidi ya miaka kumi iliyopita Yanga haijawahi kufungwa na Toto iwe ndani au nje ya Dar es Salam. Kama Yanga watalibeba kombe hilo leo watakuwa wamekabidhiwa rasmi kikanuni na Shirikisho la Soka la Tanzania litapaswa kutengeneza kombe lingine.

Hata hivyo viongozi wake wamekuwa wajanja baada ya kusisitiza kuwa hawaamini kama wao ni mabingwa mpaka watakapoifumua Mbao kwenye mchezo wao wa mwisho, huku wakiisikilizia rufaa ya Simba Fifa.

Mabosi wa Yanga wanaamini kuwa kama watani zao Simba wataamua kukomaa kusaka pointi za chee Fifa ni wazi ni lazima washinde mechi zote mbili tena kwa idadi kubwa ya mabao ili kujiweka salama hata kama Fifa itaamua kuibeba Simba.

Kama Yanga itashinda itafikisha pointi 68 ambazo zinaweza kufikiwa na Simba iwapo itashinda pambano lao la mwisho dhidi ya Mwadui Jumamosi hii, lakini bado Yanga ina mabao mengi ambayo Simba inaweza kuyapata kwa miujiza ambayo kama ikitokea huenda hata Fifa wakaja Dar es Salaam kuchunguza.

MSIKIE

MKWASA

Akizungumza na Mwanaspoti Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwassa, alisema katika kuelekea mchezo wa leo dhidi ya ndugu zao Toto African, watashuka kwa akili ya kusaka pointi tatu na si vinginevyo wakijiweka sawa kwa kuwa mabingwa wa mara tatu mfululizo wa ligi.

Mkwassa alisema wamekubaliana ndani ya Yanga kuwa ushindi wa timu yao hautatafutwa kwa Toto pekee bali wanataka kuhakikisha wanashinda mpaka mechi ya mwisho kukwepa mtego wa watani wao Simba.

Katibu huyo ambaye ni kiungo na kocha wa zamani wa timu hiyo, alisema Yanga inasubiri majibu ya mpango wa Simba kupeleka maamuzi yao Fifa hivyo ili kujiweka salama ni lazima washinde mechi zote na kumaliza ligi wakiwa na pointi 71.

“Viongozi tuna mtazamo tofauti, tuna lengo la kutaka kushinda mechi zote zilisalia tena kwa mabao mengi, akili ya kujipanga namna hiyo hatutaki kuingia katika mitego rahisi ya wenzetu, tumewasikia wakisema wanaenda Fifa.”

Simba inakimbilia Fifa kudai pointi za mezani za mwchi yao dhidi ya Kagera Sugar kwa madaim ilimchezesha mchezaji mwenye kadi tatu za njano.