Yanga walikuwa wale nyingi tu

Muktasari:

  • “Yanga iko vizuri katikati na mbele lakini ukiishambulia kwa mipira ya kushtukiza unakuwa umeipa wakati mgumu, safu yao ya ulinzi si imara sana.
  • “Tuliwabana pia katika mipira ya krosi, hawakuweza kupiga krosi nyingi na pia mabeki wangu wa kati walikuwa makini kuondoa hatari ambazo ziliingia ndani,” alifafanua kocha huyo ambaye amekuwa ndani ya Azam muda mrefu.

KOCHA wa muda wa Azam, Iddi Cheche amesisitiza kwamba Yanga walikuwa wale goli nyingi sana na alijua hilo ndio maana akawa anajiamini tangu awali.

“Yanga iko vizuri katikati na mbele lakini ukiishambulia kwa mipira ya kushtukiza unakuwa umeipa wakati mgumu, safu yao ya ulinzi si imara sana.

“Tuliwabana pia katika mipira ya krosi, hawakuweza kupiga krosi nyingi na pia mabeki wangu wa kati walikuwa makini kuondoa hatari ambazo ziliingia ndani,” alifafanua kocha huyo ambaye amekuwa ndani ya Azam muda mrefu.

AZAM MIL 10

Kama ulikuwa hufahamu ni kwamba kipigo cha Yanga juzi Jumamosi kilichagizwa na ahadi ya Sh 10 milioni ambayo walipewa wachezaji wa Azam kama wataifunga timu hiyo ya Jangwani.

Mabosi wa Azam waliamua kuwatia ndimu wachezaji kwa ahadi hiyo ya mkwanja ambapo kama wangepata sare wangepewa kiasi cha Sh 5 milioni lakini walikomaa na kuhakikisha wanapata ushindi na kuondoka na mkwanja mrefu.

HAIJAWAHI KUTOKEA

Kocha Mzambia, George Lwandamina ameanza na mkosi katika klabu ya Yanga ambapo amejikuta timu yake ikifungwa mabao 4-0 na Azam ikiwa ni kipigo kikubwa zaidi kwa timu hiyo tangu ilipofungwa mabao 5-0 na Simba miaka mitano iliyopita.

Yanga ilifungwa na Simba mwezi Mei 2012 na tangu hapo imekuwa na mwenendo mzuri kwani licha ya kukutana na timu kutoka nchi mbalimbali zikiwemo TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Al Ahly ya Misri haikuwahi kufungwa mabao 4-0 kama ilivyotokea kwa Azam juzi.

Azam ilipata mabao yake kupitia kwa John Bocco, Joseph Mahundi, Yahya Mohammed na Enock Agyei na kufanikiwa kumaliza ikiongoza Kundi B la michuano hiyo ya Kombe la Mapinduzi.

Lwandamina ambaye ndiye kocha bora namba tatu Afrika, amevunja rekodi ya mtangulizi wake Hans Van Pluijm ambaye katika kipindi chote cha miaka miwili ambacho ameifundisha Yanga hakuwahi kufungwa na timu pinzani mabao zaidi ya matatu tena mara mbili ambapo alifungwa na Medeama ya Ghana kwa mabao 3-1 kipigo ambacho pia alipokea kutoka kwa TP Mazembe

Mara ya mwisho Yanga kufungwa mabao mengi na timu ya Tanzania ilikuwa Septemba 2013 ilipofungwa mabao 3-2 na Azam pia. Kabla ya hapo Yanga ilifungwa mabao 3-0 na Mtibwa Sugar, Septemba 2012.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema; “Tumepata fundisho kwa kipigo, wachezaji walicheza kwa kujiachia na hilo limesababisha turuhusu mabao mengi, tunajipanga kufanya vizuri katika mechi ijayo.”